Na Byarugaba Innocent,Pwani
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge ameagiza kusitishwa kwa shughuli zote zinazohukumu vyanzo vya maji kwenye mto Ruvu pamoja na kudhibiti uvamizi wa Mto Ruvu.
Amesema kuwa shughuli zote zinazofanywa kwenye vyanzo vya Mto Ruvu kinyume na sheria zinaathiri upatikanaji wa maji kwa wananchi wa Mikoa ya Pwani na Dar.
Kunenge pia ameeleza kuwa kulingana na utabiri wa hali ya hewa uliotolewa hivi karibuni na Mamlaka ya hali ya hewa nchini kwa kipindi hiki nchi imetabiriwa kupata mvua za chini ya matarajio hivyo wananchi watumie maji kwa uangalifu na waweke akiba ya maji ya muda yatakayotumika muda mrefu.
Kunenge ametoa wito huo wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kuelezea uharibifu wa vyanzo vya maji unaofanywa na wakulima na wafugaji kwenye Mto Ruvu wanaofanya shughuli bila kuzingatia taratibu zinatakiwa kisheria
"Nitoe rai kwa wananchi wa Mikoa ya Pwani na Dar es Salaam kuanza kutumia maji kwa uangalifu kwa kuacha kutumia maji kumwagilia bustani na kufanya shughuli za kilimo," amesema Kunenge.
Aidha, amefafanua kuwa hii ni tahadhari ya awali kwa wananchi wote kuhusu hali ya upatikanaji wa maji, kwa sasa bado hali ya upatikanaji wa maji iko vizuri kwenye maeneo yote.
"Lakini pia tunachukua tahadhari hizi za awali ili kuepuka athari zilizotokea mwaka jana za upungufu wa maji zilizosababishwa na shughuli za wakulima na wafugaji kwenye vyanzo vya maji," ameongeza.
Wakati huohuo Kunenge ameipongeza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam- DAWASA kwa kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu katika jitihada za kudhibiti shughuli zinazofanywa na wakulima na wafugaji kwenye chanzo cha Mto Ruvu ambao ndio tegemeo la chanzo cha Maji katika Jiji la Kibiashara la Dar-es-Salaam na Pwani.
Haki Zote Zimahifadhiwa