Na Byarugaba Innocent,Kibaha.
Wananchi wa Halmashauri ya Mji Kibaha,Mkoani Pwani wamekuwa na mwitikio chanya wa kuhakikisha kuwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano wanapata chanjo ya Polio awamu ya tatu iliyoanza kutolewa Kitaifa tarehe 1 hadi 4 Septemba,2022.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imekuwa mratibu Mkuu wa Zoezi hili Kitaifa kwa kutoa chanjo kwa njia ya Matone ili kutokomeza Polio baada ya kuonekana viashiria vya mlipuko katika nchi jirani ya Malawi huku ikijiwekea lengo la kuwafikia watoto 12,386,854
Aidha,Halmashauri ya Mji Kibaha imetekeleza Zoezi hilo sambamba na Halmashauri nyingine 184 ilikuwa na lengo la kutoa chanjo kwa watoto 38,748 kwenye kata 14 na Mitaa 73 hata hivyo imeweza kuvuka lengo na kuwafikia watoto 50,313 sawa na 134 asilimia kukiwa na ongezeko la watoto 11,565 ya makadirio ya awali.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dkt.Tulitweni Mwinuka amewashukuru na kuwapongeza wananchi kwa kuhamasika na kuhakikisha kuwa watoto wao wanapata chanjo hiyo muhimu itakayotoa Kinga ya kupata magonjwa ya viungo na ulemavu ambao huwaingiza kwenye wimbi la umaskini kutokana na gharama kubwa za kuwatibia
Kwa upande wake mratibu wa chanjo wa Halmashauri ya Mji Kibaha Hope Rutatina amesema kuwa uhamasishaji kwa njia ya Matangazo na mitandao ya Kijamii,Usimamizi mzuri kuanzia ngazi ya chini,ushirikiano wa watoa huduma na kujitoa wakati wa kutekeleza Zoezi mara zote kumeifanya Halmashauri kukamilisha kwa kishindo Zoezi hilo mpaka kufikia 134.2 asilimia.
Haki Zote Zimahifadhiwa