Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imeadhimisha Siku ya Afya na Lishe katika Zahanati ya Mwenda Pole, kwa lengo la kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuzingatia afya na lishe bora kwa familia.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali pamoja na wananchi wa kata hiyo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Catherine Saguti.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Dkt. Saguti amewahamasisha kina mama kuendelea kujali na kufuatilia afya zao pamoja na afya za watoto wao mara kwa mara.
Alisisitiza umuhimu wa kuhudhuria kliniki kwa wakati ili kuhakikisha mama na mtoto wanakuwa na afya njema.Aidha, aliwapongeza kina mama kwa kuwa mstari wa mbele katika kuhudhuria huduma za afya na kuwahimiza wazazi wa kiume kushiriki kikamilifu kwa kuongzana na wenza wao kwenda hospitalini . Alieleza kuwa ushiriki wa wanaume una mchango mkubwa katika kuboresha afya ya familia.Katika hotuba yake,
Mganga Mkuu amewakumbusha wananchi kuhusu umuhimu wa kukata bima ya afya kwa familia nzima. Alieleza kuwa bima ya afya husaidia kurahisisha upatikanaji wa matibabu kwa mama, baba, na watoto bila changamoto za kifedha.Vilevile, katika maadhimisho hayo, unga wa uji wa lishe ulitolewa kwa wazazi, sambamba na elimu ya namna ya kuutengeneza kwa usahihi.
Hatua hiyo ililenga kuimarisha lishe bora kwa watoto na familia kwa ujumla.Kwa upande wake, Diwani wa Kata hiyo, Omary Baru, alisema wananchi wa kata yake wanazingatia masuala ya afya na wako tayari kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Mganga Mkuu.
Pia ameishukuru Serikali chini ya Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha sekta ya afya, pamoja na kumpongeza Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha kwa juhudi zake.
Haki Zote Zimahifadhiwa