Na Mwandishi Maalum,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo ameelekeza majengo yote ya Serikali yanayojengwa katika eneo la Mtumba jijini Dodoma kuwekewa mfumo wa kuvuna maji ya mvua ili kuepusha athari za kimazingira.
Ametoa maelekezo hayo alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo jipya la Ofisi ya Makamu wa Rais katika Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma leo Desemba 13, 2022.
Amesema ameridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo ikiwemo utekelezaji wa maelekezo ya kuweka mifumo ya uvunaji maji ya mvua aliyotoa alipokagua ujenzi huo mwezi Juni mwaka huu.
Dkt. Jafo amesema kuwa kujengwa kwa mifumo ya kuvuna maji ya mvua kutasaidia yasiweze kutiririka ovyo na kusababisha mmomonyoko wa udongo hivyo kuharibu mazingira.
“Kwa kweli nimefarijika sana na mnavyoendelea na utekelezaji wa mradi huu wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais nilipofanya ziara hapa nilitoa maelekezo na nimekuta mnayatekeleza maana mmejenga tanki hili la lita laki tano litakalopokea maji ya mvua,” amesema Dkt. Jafo.
Aidha, Waziri Jafo ametoa rai kwa mkandarasi anayejenga jengo hilo kumaliza kazi zilizobakia kwa wakati ili jengo hilo liweze kukamilika ndani ya muda uliobaki.
Awali akiwasilisha taarifa ya mradi huo Mhandisi wa SUMA JKT Sajidu Bwikizo amesema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 50 kwa mujibu wa mpango ambapo umefikia hatua ya usukaji wa nondo na umwagaji wa zege hadi sakafu (floor) ya sita.
Pia, Msimamizi wa Mradi, Meja Benedict Meena ameahidi kuyafanyia kazi maelezo ya waziri kwa kuweka mafundi wa kutosha katika kila sakafu ili kazi hiyo ifanyike na kukamilika kwa wakati.
Ikumbukwe kuwa ujenzi wa jengo hilo unasimamiwa na Mshauri elekezi Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kutekelezwa na Mkandarasi SUMA JKT.
Haki Zote Zimahifadhiwa