Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Halmashauri ya Mji Kibaha kupitia Zahanati ya Mwendapole iliyopo Kata ya Kibaha imeratibu jopo la Wakunga wabobezi wanaotarajia kutoa Elimu kwa wajawazito Alhamisi Aprili 6, 2023 ili kunusuru afya ya Mama na Mtoto wakati na baada ya kujifungua.
Prisca Nyambo ni msimamizi wa huduma za uzazi Kibaha ambaye pia ni Mkunga mbobezi ametaja huduma zitakazotolewa kuwa ni uchunguzi wa kina na Maendeleo ya Ujauzito,Maandalizi ya Kujifungua,Uchunguzi wa dalili za hatari kwa mjamzito,lishe bora,upimaji wa vipimo mbalimbali pamoja na kutoa ushauri.
Nyambo amesema Zahanati ya Mwendapole imekuwa na wateja wengi wa kujifungua kutokana na huduma bora zinazotolewa kwani takwimu zinaonesha kuwa kati ya wajawazito 140-180 hupokewa kwa Mwezi kuanza huduma za Kliniki.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha amesema nia ya Serikali ni kupunguza ama Kuondoka kabisa vifo kwa wajawazito na watoto hivyo ametoa rai kwa Wakunga wote kuwa karibu na wajawazito na wawe na kanzi data maalum itakayowasaidia kuwafuatilia
Diwani wa Kata ya Kibaha Mhe.Goodluck Manyama ameishukuru Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kupitia Halmashauri ya Mji Kibaha kwa kufanya zoezi hili na kwamba linakwenda kutoa uhakika wa afya za Watoto watakaozaliwa
Halmashauri ya Mji Kibaha yenye hospitali,Vituo vya afya na Zahanati 25 zinazotoa huduma ya Mama na Mtoto,kwa Mwezi hupokea kati ya akina mama 600-650 wanaofika kujifungua.
Haki Zote Zimahifadhiwa