Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Abubakar Kunenge amewaongoza mamia ya wananchi wa Mkoa huo kufanya usafi wa Mazingira kwenye Kituo cha afya Mkoani kama sehemu ya maadhimisho kwenye kumbukizi ya siku ya mashujaa inayofanyika kila Mwaka Julai 25.
Aidha, baada ya kukamilisha zoezi hilo aliwaongoza Wananchi kwenda kwenye mnara wa kumbukumbu kwa ajili ya uwekaji wa silaha za jadi zilizotumiwa na mashujaa hao kwenye mapambano dhidi ya wakoloni kwenye harakati za kujikomboa.
Awali dua na sala zilitolewa ambapo Shekhe wa Mkoa wa Pwani Abbasi Mtupa mashujaa hawa waliuawa kwa kutetea nchi na sio mtu na Mali yake hivyo mbele za Mwenyezi Mungu ni mashahidi na amewaombea wafunguliwe milango ya rehema kwani nguvu zao,damu zao,nafasi zao ndizo zilizobakisha amani na utulivu ndani ya Tanzania.
Mwenyekiti wa kamati ya amani Wilaya ya Kibaha Askofu Emmanuel Mhina ametumia fursa hiyo kuziombea familia za mashujaa hao neema mbele za Mungu ili ziendelee kuwa na amani na utulivu mara zote.
Dr.Gabriel Mziwanda ambaye ni Katibu wa Chama cha Kijamii (CCK) ameunga mkono suala la kuadhimisha kumbukizi ya mashujaa hawa wazalendo na kwamba kando ya kuwa yeye ni mpinzani lakini hili ni jambo jema la kupigiwa mfano.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Kibaha Mhe.Mussa Ndomba amesema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa mashujaa hawa walilitumikia na kulipigania Taifa kizalendo hivyo amani tunayoiona Sasa ni matunda yao na kwamba kuwaenzi ni jambo linalotakiwa kuwa endelevu kama sehemu ya kuhamasisha uzalendo kwenye jamii na Taifa kwa Ujumla
Maadhimisho haya yalitamatishwa na uwekaji wa silaha za jadi ambapo Mhe.Kunenge ameweka Mkuki na Ngao, mshauri wa Mgambo Kanal Erick David Mziray ameweka Sime huku Katibu tawala wa Mkoa Mhandisi Mwanasha Tumbo akiweka shada la Maua.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhe.Mussa Ndomba ameweka Shoka na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Sara Msafiri ameweka upinde.
Haki Zote Zimahifadhiwa