Na Byarugaba Innocent,Pwani
Kiwango cha maambukizi ya VVU-UKIMWI Mkoani Pwani yameendelea kushuka kutoka 5.9 hadi 5.5 ,ameeleza Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Sarah Msafiri wakati wa Maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani inayofanyika kila tarehe mosi,Disemba huku Mkoa wa Pwani ukifanyia kwenye Viwanja vya Mtongani Mlandizi,Kibaha Vijijini.
DC Msafiri aliyekuwa mgeni rasmi akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Abubakari Kunenge amebainisha kuwa kiwango hicho kimepungua kati ya Mwaka 2012-2017 ingawa Halmashauri za Kibaha Mjini,Mkuranga na Chalinze zinaendelea kuwa na maambukizi makubwa kutokana na mwingiliano wa watu kutoka maeneo mengine kwa sababu mbalimbali ikiwemo biashara.
Aidha,Msafiri amesema takwimu zinaonesha kuwa kundi la Vijana na wanaume mwamko wa kupima afya ni hafifu hali inayopelekea kugundulika na Maambukizi wakiwa na hali mbaya huku takwimu zikionesha kuwa kati ya Mwezi Januari na Novemba maambukizi mapya ya Vijana wenye umri kati ya miaka 15-24 yakifikia 1004
Dkt.Sisty Moshi kutoka THPS amesema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Mkoa wa Pwani kupambana na janga hili kwa miaka 10 Sasa na kwamba hali ya upimaji imefikia 95 asilimia huku wanaotumia dawa za kufabaza wakifikia 50,000 sawa na asilimia 98 ambapo kwa Mwaka huu wa fedha 2022/2023 kiasi cha fedha shilingi Bilioni 3.2 kimeshatolewa kwenye Halmashauri kuwezesha mapambano hayo.
Katika hatua nyingine,Halmashauri ya Mji Kibaha imefanya Maadhimisho hayo kwa kuwatembelea watoto 39 kwenye Kituo cha UMRA OPHANAGE CENTRE kilichopo kata ya Pangani na kuwapa misaada ya kibinadamu ikiwemo chakula.
Siwema Cheru, mratibu wa UKIMWI Halmashauri ya Mji Kibaha amesema mahitaji hayo yamegharimu kiasi cha shilingi milioni tatu zilizotokana na Makusanyo ya Mapato ya ndani ya Halmashauri.
Kaimu Katibu tawala wa Mkoa wa Pwani Rukhia Muwango amewashukuru wadau wote kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kupambana na janga hili kwa kuboresha Mazingira ya afya na huduma zake na ametumia fursa hiyo kutoa rai kwa wanaogundulika kutlhidhuria kliniki kupata nasaha na ushauri wa madaktari na kutumia dawa za kufabaza makali bila kukata tamaa.
KAULI MBIU ya Mwaka huu ni;IMARISHA USAWA.
Haki Zote Zimahifadhiwa