Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Katibu tawala wa Mkoa wa Pwani Zuwena Omary amewaelekeza watumishi wa Halmashauri ya Mji Kibaha kufanyakazi kwa bidii,weledi na kufuata misingi ya Sheria,Kanuni,taratibu na miongozo iliyopo ili kuisaidia Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ya kuwahudumia wananchi na kuwapelekea Maendeleo.
Zuwena ameyasema hayo Septemba 9,2022 kwenye kikao cha wataalam kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi alipofika kujitambulisha na kuzungumza na watumishi hao ambapo pamoja na mambo mengine ametumia fursa hiyo kuweka mikakati ya kuendelea kuufanya Mkoa wa Pwani kung'ara kwenye mambo ya Kitaifa ikiwemo ukusanyaji wa Mapato.
"Watendaji wenzangu tunawajibu wa kutekeleza kwenye Serikali sawa na Majukumu ambayo tumeomba kuyatekeleza,nchi yetu ndio kila kitu kwetu.Uzuri wa Tanzania ni wetu na changamoto ni zetu lakini sisi ndio wenye uwezo wa kuzitatua ili Tanzania iendelee kusonga mbele.Wewe ndio injini na Maendeleo kwenye Taifa hili"...amesema Zuwena.
Aidha,Zuwena ameongeza kuwa Mtanzania unapolegalega kwa sababu yoyote Ile kwa majukumu uliyopewa ya upangaji,utekelezaji na Usimamizi kwa vyovyote vile hatutakwenda sawa na Mipango ya nchi hivyo ametoa rai kwa watumishi kufanyakazi pasipo kuwa na visingizio vyepesi vya ukosefu Magari,Ukubwa wa maeneo ya kazi kiutendaji,ufinyu wa bajeti na kwamba hizo ni changamoto za Kawaida zinazotakiwa kutafutia ufumbuzi bila kuathiri malengo yaliyopangwa kutekelezwa kwa maslahi ya nchi yetu.
Katika hatua nyingine Katibu tawala huyo amewapongeza menejimenti kwa kuweka mikakati na na inayotekelezeka iliyofanya kukusanya Mapato ya ndani kwa 132 asilimia yatakayotumika kuwapelekea wananchi MaendeleoAwali Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde amemweleza Katibu tawala huyo kuwa menejimenti imekuwa na utaratibu wa kukutana kila wiki kutathmini ukusanyaji wa Mapato unavyoendelea kwenye kila chanzo,kubaini changamoto na kupanga mikakati thabiti ya utekelezaji ili kufikia malengo ya Kitaifa ya ukusanyaji wa Mapato.
Hii ni mara ya kwanza kwa Katibu tawala huyo kufika kujitambulisha na kuongea na watumishi tangu alipoteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchukua nafasi ya Mhandisi Mwanasha Tumbo.
Haki Zote Zimahifadhiwa