Na Mwandishi wetu, Mwanza
Serikali imewataka Watendaji wa Halmashauri nchini kufanya tathmini ya rasilimali zilizopo kwenye vituo vya afya 234 vinavyojengwa kwa fedha za Tozo ili kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno.
Kauli hiyo ya Serikali imetolewa na Dkt. Grace Magembe Naibu Katibu Mkuu (AFYA) Ofisi ya Rais TAMISEMI wakati akifunga Mkutano wa Madaktari wa Afya ya Kinywa na Meno wa Mikoa Tanzania Bara leo Novemba 22, 2022, uliofanyika katika Ukumbi wa TMDA, Jijini Mwanza. Dkt. Magembe ameongea kwa njia ya Mtandao (Zoom).
“vituo vya afya 234 vya Tozo vinavyojengwa kuna vyumba mahsusi kwa ajili ya kutoa huduma za afya ya Kinywa na Meno, natoa maelekezo kwa Halmashauri zote kutathmini rasilimali walizonazo na kuwekeza katika vituo hivi hususan vile ambavyo kuna mahudhurio makubwa ya wateja” amesema Dkt. Magembe.
Dkt. Magembe amesema Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kuboresha huduma za afya ya kinywa na meno, kuratibu huduma za afya ya msingi kulingana na Sera na Miongozo iliyopo pamoja na hatua nzuri iliyofikiwa mpaka sasa ambapo huduma hizo zinatolewa kwenye hospitali za Halmashauri 159 sawa na asilimia 86 ikilinganishwa na asilimia 56 mwaka 2019.
Aidha amesema jumla ya vituo vya afya 173 vikiwemo vituo 164 vya serikali na vituo 9 vya mashirika ya dini vinatoa huduma kwa sasa sawa na ongezeko la vituo 46.
Aidha, amesema Serikali imeajiri watumishi 145 wa afya ya kinywa na meno kwa ajili ya huduma za afya ya msingi wakiwemo matabibu wa meno 142 na madaktari wa kinywa na meno watatu waliajiriwa sambamba.
Dkt Omary Chande Mwenyekiti wa Madaktari wa Afya ya Kinywa na Meno wa Mikoa Tanzania Bara maagizo yote watayatekeleza kama ilivyoagizwa na Serikali lakini pia ameshukuru kutengwa bajeti ya vifaa tiba shilingi Bilioni 7.1 pamoja na ujenzi wa vituo vya afya vya kimkakati ambapo Bilioni 1.7 zimekwishapelekwa kwenye Halmashauri.
Mkutano huo wa siku mbili ulifunguliwa mapema jana na kauli mbiu yake inasema “Mchango wa Takwimu bora za afya ya Kinywa na Meno katika kufikia maamuzi na utekelezaji” inayosisitiza matumizi ya takwimu bora na kufanya maamuzi sahihi yenye tija katika utoaji wa huduma za afya ya Kinywa na Meno nchini.
Haki Zote Zimahifadhiwa