Na Byarugaba Innocent,Pwani
Halmashauri ya Mji Kibaha,Mkoani Pwani inaendelea na ukamilishaji wa ujenzi wa Vituo vya afya viwili,Zahanati mbili na nyumba ya Mtumishi kwenye Kata za Pangani,Kongowe,Tumbi na Misugusugu zitakazogharimu kiasi cha fedha shilingi 1,253,625,070 kutoka kwenye vyanzo tofauti vya Mapato.
Mganga Mkuu wa Halmashauri Dr.Tulitweni Mwinuka ameeleza kuwa fedha za ujenzi zinatoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo miamala ya simu kiasi cha milioni 500,000,000 Mapato ya ndani milioni 435,000,000,TASAF milioni 183,928,570,Serikali kuu milioni 100,000,000 na wananchi wakichangia milioni 34,696,500 na kufanya jumla ya fedha yote kufikia 1,253,625,070
Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Kibaha John Alexander amesema kuwa Majengo hayo yatakayo wanufaisha walengwa kati ya 16,500-33,000 kwa Mwaka yanajengwa kwa mfumo wa 'force account' na yanatarajia kukamilika Mwezi Septemba,2022
Anitha Lyoka,mratibu wa TASAF Kibaha Mji amesema kuwa TASAF hutekeleza majukumu manne ya Msingi ikiwemo uhawilishaji wa fedha kwa kaya za walengwa,ujenzi wa miundombinu,kuhamasisha uwekaji wa akiba ili kukuza uchumi wa kaya na utekelezaji wa miradi ya Kijamii ambapo kwa Mwaka 2022/2023 wameanza na ujenzi wa Zahanati ya Mwanalugali pamoja ya nyumba watakayoishi watumishi wawili kwenye Zahanati ya Vikawe.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde amewashukuru wadau wote wa maendeleo hasa kwenye sekta ya afya kuona umuhimu wa kuongeza Vituo vya afya, Zahanati na nyumba ya Mtumishi ambavyo vinakwenda kuhudumia afya ya mwananchi kwani taifa lolote Duniani hutegemea nguvu kazi iliyo imara ili liweze kuzalisha na kujenga uchumi wake.
Haki Zote Zimahifadhiwa