Na Byarugaba Innocent,Pwani
Waziri wa ardhi,nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Anjelina Mabula pamoja na Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mheshimiwa Mashimba Ndaki kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mheshimiwa Abubakar Kunenge wamefikia pazuri kuhitimisha Mgogoro wa eneo la Mitamba kiwanja namba 34 linalovamiwa na wananchi tangu Mwaka 2007 ilihali likiwa linamilikiwa kihalali na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Kwa vipindi tofauti wavamizi hao wameendelea kumega eneo hilo la Wizara na kujimilikisha kwa kujenga Makazi ya kudumu na wengine wakiwauzia wananchi na taasisi zikiwemo za kidini kinyume cha sheria na wavamizi 24 tayari wameshajikusanyia fedha haramu zaidi ya milioni 900 ambazo Serikali ingeweza kutolea huduma za Maendeleo kwa wananchi wenyewe
Dalili za kutamatishwa kwa Mgogoro huo na kukomesha vitendo vya uvamizi wa maeneo umebainishwa na kamati iliyoundwa na Wizara ya Ardhi ikiongozwa na Kamishna msaidizi wa Polisi Peter Matagi iliyowasilishwa mbele ya mawaziri hao na kuonesha kuwa wananchi waliingia kimakosa kwenye eneo hilo kwa kuvamia,kununua kinyemela pasipo kufuata taratibu za kisheria kuanzia miaka ya 1988 lilipotwaliwa na Wizara kwa kuwalipa fidia zaidi ya wananchi 1500 walikuwemo kwenye eneo hilo lenye Ukubwa wa Hekta 4000.
Hussein Sadick Kamishna msaidizi wa ardhi Mkoa wa Pwani aliyekuwa Katibu wa kamati amesema kuwa Mwaka 2007 Wizara na Mifugo na Uvuvi ilifanya tathmini ya eneo lake na kugundua kuwa wavamizi wameshavamia eneo kubwa hivyo ili kulinusuru Wizara ilitoa Hekta 2963 kwa Halmashauri ya Mji Kibaha kama mamlaka ya upangaji kisheria kwa ajili ya kupanga Mji huku Wizara ikibakiwa na Hekta 1037 na kuzipima.
Aidha,Sadick ameongeza kuwa wakati wa tathmini ya maendelezo ya wavamizi jumla ya mabanda ya tope,miti na nyasi 208,Mapagale 442,nyumba za chumba kimoja 239,nyumba zilizokamilika ujenzi 80 na nyumba zenye Makazi 46 na kufanya jumla ya maendelezo 1015 zilibainika
Sadick amesema kuwa wavamizi 1611 walioitwa kuhojiwa,1156 walisema wamenunua ndani ya kiwanja Namba 34 kati yao 1002 waliwasilisha mikataba ya kughushi ya mauziano,154 hawakuwa na nyaraka,403 walikiri kuwa wamevamia baada ya kuona wenzao wanavamia, 46 walipewa na wavamizi waliotangulia na 6 wamerithishwa.
"Mhe.Waziri wavamizi hawa wamevamia wakiwa na ufahamu kuwa wanavamia kwa kuhimizana kujenga kwa kusema kuwa Serikali mwishowe itawaachia Ardhi yao"alisema Sadick
Hata hivyo mapendekezo ya kamati ni kupangwa upya kwa eneo hilo kwa kuzingatia mahitaji ya taasisi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Mji Kibaha yenye mamlaka kisheria,kuwashitaki wavamizi wote kwa kitendo cha kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na walioandaa nyaraka za kughushi wachukuliwe hatua za kisheria ili kukomesha tatizo sugu la uvamizi wa maeneo
Aidha,Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha ameelekezwa kufuta pimaji na Vibali vya ujenzi vilivyotolewa ndani ya kiwanja hicho.
Kwa pamoja Waziri wa ardhi Dkt.Anjelina Mabula pamoja na Mashamba Ndaki Waziri wa Mifugo na Uvuvi wamebariki mapendekezo yote na kamati kufanyiwa kazi haraka huku wakitoa rai kwa wananchi kwenda kwenye Halmashauri kijiridhisha wanapotaka kununua Ardhi halali wanapokuwa na uhitaji na si vinginevyo
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakar Kunenge amesema wakati wa kuanza kwa kampeni ya kutokomeza Migogoro ya Ardhi Mkoa wa Pwani waliahidi kufanya kazi kwa uadilifu,kuzingatia sheria na kwamba kutokana na taarifa hiyo haki itatendeka,hakuna atakayeonewa na hakuna atakayependelewa.
Mapema Mwaka huu Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Samia kupitia Wizara ya Ardhi imeikopesha Halmashauri ya Mji kibaha kiasi cha fedha Bilioni 1.588 kwa ajili ya kutambua,kupima,kupanga na kuwamilikisha wananchi kwa bei nafuu ya shilingi 1500 kwa kila mita ya Mraba.
Haki Zote Zimahifadhiwa