Kibaha, 10 Julai 2025
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amekutana na wadau na wamiliki wa viwanja vilivyoko katika eneo la Mji wa Kati (Central Business District - CBD) Kibaha Mjini, katika kikao kilicholenga kuimarisha ushirikiano na kuweka mikakati ya pamoja ya uendelezaji wa maeneo hayo.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Manispaa na kuhudhuriwa na wamiliki wa viwanja kutoka maeneo mbalimbali ya CBD, maafisa kutoka idara ya ardhi.
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Shemwelekwa amesema Halmashauri ya Kibaha imepanda hadhi na kuwa Manispaa rasmi kuanzia tarehe 20 Juni 2025, hatua inayoweka msukumo mpya kwa maendeleo ya manspaa ya kibaha.
“Kupanda kwa hadhi ya Kibaha kuwa Manispaa ni fursa na wajibu mkubwa. Tunahitaji kuona mabadiliko ya kweli katika muonekano wa mji wetu , viwanja vinapaswa kuendelezwa kwa kasi, kwa mpangilio, na kwa kuzingatia sheria zote za mipango miji na ujenzi,” alisisitiza Dkt. Shemwelekwa.
Ameongeza kuwa Manispaa imewawekea wamiliki wote wa viwanja muda wa miezi sita kuanza rasmi shughuli za ujenzi katika maeneo yao, na kuonya kuwa wasiotekeleza agizo hilo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za ardhi na mipango miji.
Aidha, Dkt. Shemwelekwa amewahimiza wamiliki wa viwanja kushirikiana na watumishi wa idara ya ardhi kwa ukaribu ili kuhakikisha wanapata taarifa sahihi na kuepuka kudanganywa na watu wasio rasmi au vishoka.
Kwa upande wao, wamiliki wa viwanja wamempongeza Mkurugenzi Kwa juhudi za kupandisha hadhi kuwa Manispaa. Mzee Mfinanga ( Njuweni), akizungumza kwa niaba ya wadau waliokuwepo, amesema
“Tunampongeza Mkurugenzi kwa uongozi wake na dhamira ya dhati ya kuujenga mji wa Kibaha. Sisi kama wamiliki tupo tayari kushirikiana kwa vitendo ili kufanikisha malengo haya ya pamoja.”
Kikao hicho kimeelezwa kuwa sehemu ya mpango wa Manispaa wa kuimarisha Manspaa ya Kibaha kuwa kitovu cha biashara, huduma na makazi bora, sambamba na ajenda ya maendeleo ya miji ya kisasa nchini.
Haki Zote Zimahifadhiwa