Na. Innocent Byarugaba, Kibaha
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Jenifa Omolo amekabidhiwa Mashine ya Mionzi na vifaa vyake aina ya Cytec Digital Machine kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya Kibaha iliyopo Mtaa wa Lulanzi kutoka kwa Mtaalam wa kufunga mashine hiyo Mhandisi Onesmo Mvanga.
Mashine hiyo iliyonunuliwa na Wizara ya Afya kutoka kampuni ya Cytec Digital mashine yenye makao yake makuu nchini Korea Kusini ina uwezo mkubwa wa kufanya kazi kutegemeana na idadi ya wagonjwa watakaofika kupata huduma za kitabibu hata zaidi ya 200 kwa siku.
Omolo ameishukuru sana Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Dkt.John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya nchini na kwamba ametoa rai kwa wagonjwa kufika kupata huduma ya mionzi hospitalini hapo badala ya kwenda hospitali ya rufaa ya Tumbi
Mhandisi Mvanga aliyesaidiana na Mhandisi Helson Mwamoto kufunga mashine hiyo, amesema kuwa “mashine hiyo ni sawa na mtambo ambao umefungwa hospitali ya Ocean Road na kwamba hauna ukomo wa kutoa huduma kwa wagonjwa kwani ni wa kiwango cha juu sana”
Aidha, amesema kuwa matengenezo yoyote yatakayojitokeza ndani ya kipindi cha miaka miwili kuanzia sasa yatafanywa na kampuni hiyo bure.
Kwa upande wake Lenganwa Samweli, mtaalam wa mionzi kutoka hospitali ya wilaya Mjini Kibaha atakayeitumia ameridhishwa na mashine hiyo na kuahidi kuitumia kwa weledi ili iweze kutoa huduma hiyo kwa wananchi muda mrefu.
Mganga mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dr.Tulitweni Mwinuka mbali ya kuishuku Serikali ametoa rai kwa wataalam wa afya kuendelea kutoa huduma za kitabibu kwa weledi huku wakizingatia sheria, kanuni na taratibu
Vifaa vingine vilivyokabidhiwa ni pamoja na Multi-tray printer, Report Printer, Protective gear lead apron, Goggles, Gonad shield, Neck shield ,Gloves pamoja na Radiation hazard warning signs
Haki Zote Zimahifadhiwa