Katika mwendelezo wa mashindano ya SHIMISEMITA yanayoendelea kufanyika jijini Tanga, Timu ya soka ya Manispaa ya Kibaha imeibuka kidedea baada ya kuichapa timu ya Halmashauri ya Manyoni kwa bao 1-0 katika mchezo uliopigwa kwenye uwanja wa shule ya msingi Kombez.
Mchezo huo ulianza kwa kasi, huku timu ya Manyoni ikionekana kuchangamka mapema kwa kuishambulia Manispaa ya Kibaha mara kwa mara. Hata hivyo, licha ya mashambulizi hayo, Manispaa ya Kibaha ilijipanga upya na dakika ya 29 ya kipindi cha kwanza ilifanikiwa kupata bao kupitia shuti kali lililomshinda kabisa mlinda mlango wa Manyoni.
Licha ya juhudi za timu ya Manyoni kusawazisha bao hilo, walishindwa kuziona nyavu za wapinzani wao hadi kipenga cha mwisho, na matokeo yakasalia Manispaa ya Kibaha 1 - 0 Manyoni.
Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Afisa Michezo wa Manispaa ya Kibaha alisema kuwa amefurahishwa na ushindi huo na ameisifu timu kwa kuendelea kuonyesha maendeleo mazuri. Aliongeza kuwa wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanafikia hatua za juu zaidi katika mashindano haya.
Mashabiki wa timu hiyo pia walionekana wakifurahia ushindi huo, wakipongeza juhudi za wachezaji na benchi la ufundi kwa kuibuka na ushindi muhimu katika hatua hiyo ya mashindano.
Mashindano ya SHIMISEMITA yameendelea kuvutia hisia kali kutoka kwa mashabiki huku timu zikionyesha ushindani mkali na nidhamu ya hali ya juu uwanjani.
Haki Zote Zimahifadhiwa