CRDB Bank Yatoa Madawati 30 kwa Shule ya Sekondari Viziwaziwa Kupitia Programu ya “Keti Jifunze”
Kibaha, Pwani – Katika kuunga mkono juhudi za serikali kuinua sekta ya elimu nchini, Benki ya CRDB imetoa msaada wa madawati 30 kwa Shule ya Sekondari Viziwaziwa kupitia programu yake ya kijamii “Keti Jifunze”. Msaada huo umetolewa kama sehemu ya mkakati wa benki hiyo kusaidia maendeleo ya elimu na mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya madawati hayo, Meneja wa Kanda ya Pwani wa CRDB Bank, Bw. Badru Iddi, alisema benki hiyo inaendelea kusaidia sekta ya elimu kama njia ya kurudisha fadhila kwa jamii ya Watanzania ambao wameendelea kuiamini na kuiunga mkono benki hiyo.
“Kupitia program yetu ya Keti Jifunze, tumekuwa tukisaidia shule mbalimbali kwa kutoa madawati na vifaa vya elimu. Hadi sasa, katika Mkoa wa Pwani tumetoa jumla ya madawati 250. Lengo letu ni kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira mazuri ya kusomea ili tuzalishe viongozi bora wa baadae,” alisema Bw. Iddi.
Aidha, aliongeza kuwa msaada huu ni sehemu ya faida ambayo benki hupata kutoka kwa wateja wake, na hivyo ni njia ya kusema “ahsante” kwa Watanzania. Alisisitiza kuwa CRDB Bank itaendelea kusaidia sekta nyingine muhimu kama kilimo, afya na majanga ya dharura.
Naye Meneja wa CRDB Bank Tawi la Kibaha, Bi. Rose Kazimoto, alisema benki hiyo imejikita katika kuhakikisha kila mtoto wa Kitanzania anapata nafasi ya kusoma katika mazingira rafiki.
Kwa upande wa serikali, Renita Ruzabiko Afisa Tarafa wa Kongowe aliyepokea msaada huo kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, aliishukuru CRDB Bank kwa moyo huo wa kujitolea na kuwataka waendelee na jitihada hizo kwa shule nyingine zinazohitaji msaada kama huo.
Akizungumza Kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Isihaka Mwalimu Afisa elimu Sekondari ameishukuru CRDB Bank Kwa msaada huo Kwa kuwa unakwenda kuboresha elimu Bora.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Viziwaziwa nao hawakuficha furaha yao baada ya kupokea madawati hayo. Wamesema msaada huo umewapunguzia changamoto ya kuketi chini au kubanana darasani na wameahidi kuyatunza madawati hayo huku wakisoma kwa bidii ili kufikia ndoto zao.
#Ulipo, Tupo#
Haki Zote Zimahifadhiwa