Na Innocent Byarugaba, Kibaha
Ni takribani miezi minane tangu kukamilika kwa hospitali ya wilaya ya Kibaha, Lulanzi na kuanza kutumika kutoa huduma za kitabibu ikiwemo uzazi. Tayari watoto sita wamezaliwa akiwemo Jane Salmin mtoto wa awali kabisa kuzaliwa tarehe 4Februari 2021akiwa na uzito wa kilogram 3.6. Amepewa jina la Janerose kama ishara ya shukurani kwa mkunga aliyemzalisha kwa kumpa huduma bora, upole na unyenyekevu kwa kazi yake. Hakika Janerose anaipenda na kuijali taaluma yake!
Juni 8, 2020 Ummy Mwalimu (MB) aliyekua Waziri wa afya, maendeleo ya jamii, jinsia, wazee na watoto kipindi ch kwanza cha serikali ya awamu ya tano alipofika hospitali ya wilaya Lulanzi kufunga rasmi iliyokua kambi ya wagonjwa wa Covid-19 na kuamuru kuanza kutumika kwa matibabu ya kawaida baada ya kujiridhisha kuwa hakuna tena mgonjwa mpya.
Hata hivyo, tunaombwa kuendelea kuchukua tahadhari, sala na nyungu, kula matunda hasa yenye Vitamini C pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka kwa kutumia sabuni ama vitakasa mikono, kufanya mazoezi na kuzingatia umbali kati ya mtu na mtu ‘social distancing’
Februari 9, 2021 madiwani wa mji Kibaha wakiongozwa na mwenyekiti wa halmashauri Mussa Ndomba wanatembelea hospitali hiyo ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yao ya kawaida ya ukaguzi wa miradi robo ya pili. Wanapokelewa kwa shangwe, nderemo na bashasha toka kwa madaktari, wauguzi na watumishi wengine kwani ndio mara ya kwanza kwa wawakilishi hao wa wananchi kufika hapo tangu waliposhinda na kuchaguliwa kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba, 2020.
Mganga Mfawidhi wa hospitali Dkt. Sabinusi Ndunguru anawaeleza wawakilishi hao wa wananchi ngazi ya kata kuwa kando na huduma ya uzazi, huduma zingine zinazotolewa ni Ushauri wa Kidaktari, huduma ya macho, kliniki ya magonjwa yasiyoambukiza (NCD), upasuaji mdogo, uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi, huduma ua Ultra sound pamoja na huduma za maabara mathalan Malaria, Sukari, Mkojo, HIV, kupima vidonda vya tumbo na homa ya matumbo (typhoid)
Dkt. Ndunguru anaongeza kuwa tangu kuanza kutumika kwa hospitali hiyo, huduma za kitabibu, miundombinu ya hospitali imeendelea kuboreshwa ambapo tayari mashine ya mionzi aina ya Cytec digital yenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya watu 200 kwa siku imeshasimikwa tangu tarehe mwezi Agosti, 2020. Aidha, mashine ya dawa za usingizi imehamishwa kutoka kituo cha afya Mkoani na kupelekwa hospitali ya Lulanzi ili kuwezesha huduma za upasuaji.
“….Mhe.Mwenyekiti Hospitali ya wilaya Lulanzi imesajiliwa rasmi na kupata kibali Na.113982-3. Aidha, tayari imeshapata usajili wa NHIF Mwezi Januari hivyo wagonjwa wote wanufaikaji wa Bima ya afya wanaruhusiwa kufika Lulanzi kupata huduma za afya kwa gharama za NHIF.Aidha,hospitali hii itapunguza mlundikano wa wagonjwa kwenye kituo cha afya mkoani na hospitali ya rufaa ya mkoa,Tumbi”……anatanabaisha Dkt. Ndunguru.
Safina Zililo ni miongoni mwa watu waliofika kwa matibabu hospitali ya Lulanzi. Kando ya kutoa changamoto ya barabara na gharama kubwa ya usafiri wa bodaboda aliotozwa, anawamwagia sifa wahuduma wa afya kwa huduma nzuri wanazotoa pamoja na ushauri pale unapohitajika. Hata hivyo, anaomba taasisi zinazoshughulika barabara mijini na vijijini -TARURA na usafiri wa nchi kavu- LATRA kuangalia namna sahihi ya kushughulia kero hizo ikiwemo kuanzishwa kwa ‘route’ za daladala zitakazotoa huduma kwa watu wanaofika hospitali ya Lulanzi kwa gharama nafuu.
Kwa upande wake Selina Msenga, ambaye pia ni makamu mwenyekiti wa halmashauri, aliye pata matibabu kwenye hospitali hiyo anatoa rai kwa wananchi wa Kibaha na maeneo jirani
kufika hapo kwa ajili ya matibabu kwani licha ya kuwa hospitali ipo kwenye mandhari nzuri, hata muda unaotumika kuanzia kuingia, kumwona daktari mpaka kupata huduma ni mdogo na kwamba muda unaookolewa utatumika kwa shughuli nyingine za kujiongezea kipato.
Nawasiliana na Meneja wa TARURA Kibaha, Mhandisi Bupe Angetile kuhusu changamaoto ya barabara inayoelekea hospitali ya Wilaya Lulanzi na mikakati yake, anabainisha kuwa tayari barabara hiyo imeshatengewa fedha kiasi cha bilioni 3.6 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2021/2022 zitakazowezesha kujenga barabara kwa kiwango cha lami kilomita 3.
Jenifa Omolo ni Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Kibaha mbali na kumshukuru Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuipatia hospitali ya Wilaya anaeleza mikakati ya uendelea kuiboresha ikiwa ni pamoja na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuongeza gari la wagonjwa, kuongeza vifaa tiba, pamoja na kuongeza watumishi kwa kuishirikisha Wizara ya afya.
Kibaha mji ni miongoni wa halmashauri 67 zilizopokea fedha za ujenzi wa hospitali za wilaya. Mpaka sasa imeshapokea shilingi 1,894,419,835 zilizotumika kujenga majengo saba ya awali yanayowezesha kuanza utoaji wa huduma za kitabibu. Jengo la utawala, Jengo la wagonjwa wa nje, mionzi, stoo ya dawa, jengo la wazazi na jengo la kufulia yamejengwa kwa mfumo wa fundi jamii huku thamani ya fedha na jengo husika ukizingatiwa. Yamekamilika kwa wastani wa 99.5% -100%
Utawala wa Rais Magufuli umeleta neema ya matibabu kwa watanzania vijijini na mijini. Mbali ya kuajiri wataalam wengi kwenye hospitali mpaka zahanati, kuongeza bajeti ya dawa na vifaa tiba kutoka bilioni 31 mpaka bilioni 270, tumeshuhudia mapinduzi makubwa ya uboreshaji wa miundombinu kwenye sekta ya afya ambapo serikali imeweza kutoa zaidi ya bilioni 100,500,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali za wilaya 67. Hii ni historia mpya kwani tangu nchi ipate uhuru ilikua na hospitali za wilaya 77 tu, Serikali ya awamu ya tano kwa mwaka 2019 imefikisha hospitali za wilaya 144 tena utekelezaji wake ukifanyika ndani ya miezi sita tu.
Rais Magufuli amenunua mitambo ya magonjwa yanayohitaji utaalam mkubwa baada ya kujiridhisha kuwa serikali imesomesha wataalam wa kutosha. Mahitaji ya CT Scan, MRI, utambuzi wa DNA, upandikizaji Figo sasa unafanyika nchini. Wagonjwa hawapelekwi tena ughabuni kwani Serikali ya awamu ya tano imepambana kuhakikisha afya za watanzania zinatazamwa hapahapa huku fedha za serikali zikiokolewa
Albert Einstein, mshindi wa tuzo ya Nobel 1921, Mjerumani na mbobezi wa fizikia aliyezaliwa Machi 14,1879 na kufariki Aprili 18, 1955 alipata kusema “Jitahidi kila unachofanya kisikupe Mafanikio tu, bali kikupe thamani” Hakika Rais Magufuli ameonesha si tu mafanikio bali thamani ya Tanzania na Mtanzania mwenyewe kwenye anga la Kimataifa hasa kwenye sekta ya afya.
Mwenyekiti wa hamashauri ya Mji Kibaha Mussa Ndomba anatoa rai kwa wataalam wote wa afya kwenye Mji wa Kibaha kuendelea kumheshimisha Rais Magufuli kwa kutoa huduma bora ,kwa weledi, kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo yote ya afya huku wakiviishi viapo vyao na kamwe wagonjwa hawapaswi kuichukia hospitali kwa sababu ya huduma duni au kauli mbaya toka kwa wataalam huku akiwaomba watoe huduma zitakazowapa faraja na matumaini wagonjwa.Timizeni wajibu wenu!
Halmashauri ya mji Kibaha watu wapatao 157,695 kutokana na makadirio ya Ofisi ya taifa ya Takwimu (NBS) Mwaka 2019, ina kata 14 na mitaa 73. Aidha, ina jumla ya vituo vya afya na zahanati 44, vinavyomilikiwa na serikali ni 15 vikiwemo 7vinavyotoa huduma ya CEmONC, vituo 21 vinatoa huduma ya RCH na BEmONC ni 20.
Haki Zote Zimahifadhiwa