Na Byarugaba Innocent,Kibaha.
Jumla ya watahiniwa 3537 wa Kidato cha nne wanatarajia kuanza Mtihani wa Taifa Novemba 14,2022 kuhitimisha safari yao ya miaka minne ya masomo yao kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha.
Afisa Elimu taaluma wa Halmashauri ya Mji Kibaha Edward Jidamva amebainisha kuwa katika idadi hiyo wanaume ni 1581 sawa na asilimia 44.6 huku wanawake wakiwa 1956 sawa na asilimia 55.4 ambapo kwa idadi hiyo Mikondo 107 imeshaandaliwa.
Aidha,Jidamva amebainisha kuwa katika Mtihani huo nyeti kabisa nchini,watahiniwa 297 wa Kujitegemea wataketi kuungana na wenzao kwenye vituo 10 ambapo jumla ya mikondo nane imeandaliwa.
Akizungumzia maandalizi ya watahiniwa,Mkuu wa shule ya Sekondari Zogowale Tatu Mwambala amesema kwa Ujumla wanafunzi wameandaliwa vizuri kwani wao kama Wakuu wa shule wamekuwa na mikakati thabiti ya kuhakikisha Kibaha inafanya vizuri kwenye mitihani yote ya Taifa kwa kuwaandaa vema wanafunzi kimasomo
Kwa upande wake Afisa Elimu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Rosemary Msasi amesema hana wasiwasi na wanafunzi wote kutoka kwenye shule 40 kwani wameandaliwa vema hivyo ametoa rai kwa watahiniwa hao kujiamini wanapojibu mitihani yao na wakumbuke pia kumtegemea Mwenyezi Mungu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde amesema walimu wametekeleza wajibu wao kwa kuwafundisha kwa kipindi cha Miaka minne,Serikali imetekeleza wajibu wake wa kuweka miundombinu wezeshi,Wazazi wametekeleza wajibu wao wa kuwalea na kuwapa mahitaji Muhimu na sasa ni zamu ya wanafunzi wenyewe kutekeleza wajibu wao wa kufanya Mtihani na kufaulu hivyo amewatakia kila la kheri.
Haki Zote Zimahifadhiwa