RAS PWANI AWATAKA WATUMISHI KUCHAPA KAZI KWA KASI NA KUZINGATIA WELEDI
Na Innocent Byarugaba, Kibaha
Katibu tawala Mkoa wa Pwani, Dkt Delphine Magere amefanya ziara ya siku moja kwenye halmashauri ya mji wa Kibaha kwa lengo la kuhimiza utendaji kazi kwa watumishi huku wakizingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo yote ya utumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi.
Akiwalisilisha taarifa ya watumishi, Mkurugenzi wa halmashauri ya mji Kibaha Jenifa Omolo alisema kuwa ikama ya watumishi ni 2203 hata hivyo waliopo ni 2033 huku kukiwa na upungufu wa watumishi 170. Aidha, alisema kuwa watumishi 66 watarajiwa kuajiriwa katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwani tayari mishahara yao imeshatengwa na kuidhinishwa na Ofisi ya Raisi-Utumishi na utawala bora.
Akiongea na watumishi kwenye ukumbi wa halmshauri, Dkt. Magere alitumia fursa hiyo kuwasilisha salaam kutoka kwa mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo sanjali na kuwatakia mwaka mpya 2021 na kuwapongeza watumishi wote kwa kufanikisha ufaulu mkubwa kwenye mitihani ya kitaifa, ukusanyaji wa mapato, Viwanda na sekta nyingine kwani mafanikio hayo yanaonesha kweli halmashauri ya Mji Kibaha ni Makao makuu ya Mkoa wa Pwani huku akitoa rai ya kutojibweteka kwa mafanikio hayo zaidi ya kuongeza kasi zaidi kiutendaji.
Katika mkutano huu changamoto za watumishi ziliibuka. Juma Mkalipa na Mkaminoela Hangaya waliotaka kujua ni lini serikali itaboresha masilahi ya watumishi hasa kuongeza Mishahara na kulipa malimbikizo ambayo serikali haojalipa kwa muda mrefu
Akijibu changamoto hizo, Dkt.Magere aliwasihi watumishi wote kuwa watulivu na wavumilivu kwani serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli ni sikivu na kwamba itaongeza muda ukifika kwani kwa sasa serikali imejikita kwenye kujenga uchumi ikiwemo ujenzi wa miundombinu na itakapokamilika suala hilo litatazamwa na kwamba hii sio Pwani tu ni nchi nzima
Akihitimisha mkutano Dkt.Magere aliwasihi watumishi kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa kupendana, kutokufanyakazi kwa mazoea, kutenda kwa ubunifu utakaoongeza tija, kubuni vyanzo vipya vya mapato na kushiriki vyema kwenye ukusanyaji wa mapato huku mianya ya rushwa na upotevu ikizibwa. Aidha, amewataka watumishi kutolaumiana na kunyoosheana vidole kwenye uwajibikaji huku akisisitiza kuheshimiana na kuvumiliana kwani hakuna binadamu aliyemkamilifu mbele za mwenyezi Mungu.
Haki Zote Zimahifadhiwa