Na.Innocent Byarugaba, Kibaha
Serikali ya awamu ya tano inaamini kuwa kila mtu ana jukumu kujishughulisha kwa kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kujiletea maendeleo yake na Taifa kwa ujumla. Imani hii ndiyo chimbuko la kauli mbiu za Hapa Kazi Tu! na kuacha kufanya kazi kwa mazoea!
Aidha, ina jukumu la kuhakikisha kuwa walio wanyonge kwenye jamii wanapata fursa ya kipekee ya kustawisha maisha yao na kuondokana na unyonge wao ili kupunguza tofauti za matabaka ya kichumi. Yaani mwenye nacho na asiyekuwa nacho! Kila mtu afanyekazi. Hata maandiko matakatifu yanasisitiza kufanya kazi. Na asiyefanya kazi asile!
Mhandisi Evarist Ndikilo, Mkuu wa Mkoa wa Pwani amejiwekea utaratibu wa kufanya ziara mara kwa mara kwenye maeneo ya uzalishaji mali, ujenzi wa miundombinu na maeneo ya wafanyabiashara wadogo wadogo kuona shughuli wanazofanya, kusikiliza kero zinazowakabili na kuzitatua
Kero za kubomolewa kwa soko la Picha ya ndege, lililopo kandokando ya barabara kuu iendayo Morogoro mwanzoni mwa mwezi Februari, 2021 na changamoto za miundombinu soko la Mnarani zinampeleka Mhandisi Ndikilo na kamati ya ulinzi na usalama kutembea na kufanya mikutano ya hadhara na wafanyabiashara kwenye masoko hayo yaliyopo kwenye halmashauri ya mji Kibaha akianza na Soko la Picha ya Ndege kisha Loliondo kwa nia ileile ya kusikiliza kero zao.
Hata hivyo, safari hii ameambatana na wataalamu kutoka taasisi nyingine wezeshe kwa wafanyabiashara mathalan; wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO),wakala wa barabara nchini (TANROAD),wakala unaoshughulika na usafiri wa majini na nchi kavu (LATRA) pamoja na Shirika la maji safi na maji taka (DAWASA) kwa ajili ya kutoa majawabu kwa wafanyabiashara.
Mussa Ndomba ni diwani wa kata ya Sofu na mwenyekiti wa halmashauri anasimama mbele ya hadhara huku akishangiliwa na wahudhuriaji kwa shangwe, nderemo na vifijo kuwasilisha kero nne za wafanyabishara na maboresho ya eneo la msufini lilipohamia soko jipya lililoongeza idadi ya wafanyabiashara kutoka 150 mpaka kufikia 520.
Kwanza anaanza kwa kuwasilisha changamoto ya umeme na maji huku akiziomba mamlaka husika hufikisha huduma hizo kwa bei nafuu zitakazo wawezesha wafanyabiashara kuzipata kwa gharama nafuu
Pili Ndomba anaomba kujengwa kwa kituo kipya cha daladala kitakachoshusha na kupakia abiria eneo hilo na kuimarishwa kwa kalvati linaloruhusu magari ya mizigo kuingia kuingia kutokana na kuongezeka kwa magari yaliyochepushwa njia kupisha utanuzi wa barabara eneo la Picha ya ndege
Tatu, Ndomba anaomba kuondolewa kwa wafanyabiashara waliobakia soko la zamani kwani mazingira yake sio rafiki kwa afya na usalama wa binadamu kutokana na vumbi, mitambo iliyoegeshwa na maligahafi za ujenzi unaoendelea.
Nne, Ndomba anaomba baraka kwa mkuu wa Mkoa kuanzishwa kwa mnada wa gulio na mbuzi nyama choma, kuchangamsha soko na kuwahamasisha wanunuzi kufika kufanya manunuzi ili kuongeza mapato ya Halmashauri.
….”Mheshimiwa mkuu wa mkoa natamani sana soko hili lisimame, wajasiliamali ili hawa wadogo wapate mikopo kutoka halmashauri na taasisi nyingine za kifedha wafanye biashara zenye tija. Sisi tunataka maendeleo….Tuachane na siasa kwani kipindi cha kampeni kimepita sasa ni utekelezaji….” Anasema Ndomba.
Hata hivyo, mkuu wa mkoa wa Pwani, Mhandisi Evarist Ndikilo anakiri kupokea malalamiko ya wafanyabiashara kuondolewa kwenye eneo la Picha ya Ndege na kupelekwa mahali ambapo wanadai hakuna miundombinu ilhali wakiwa na vitambulisho vya wajasiliamali na huku wakiwa na mikopo benki hali ambayo itawafanya sio tu kukosa riziki bali itawafanya washindwe kulipa mikopo hiyo.
Mhandisi Ndikilo anabainisha sababu za wafanyabiashara kuondolewa eneo hilo lenye upana usiozidi mita 20 kuwa ni ufinyu wa eneo lenyewe, vumbi jingi linalotokana na shughuli za ujenzi unaoendelea pamoja na mitambo iliyoegeshwa, msongamano mkubwa wa watu pamoja na bodaboda, biashara ya ukaangaji wa chipsi hali inayoweza kusababisha kulipuka kwa magari yanayobeba matenki ya mafuta kama iliyotokea Morogoro miaka mitatu iliyopita na kusababisha vifo vya watu takribani 100.
“….Fedha zinatafutwa ndugu zangu, lakini roho ya mtu haipatikani popote ikishatoka ndio basi tena. Awe Mjomba, Bibi, Mama akishaondoka ameondoka. Nawapenda sana wananchi wangu”, binafsi pamoja na kamati yangu ya ulinzi na usalama hatupo tayari kuona mkipata madhara ambayo yanaonekana. Nayasema haya kwa nia njema kabisa ya kuokoa maisha yenu …
Aidha, Ndikilo anakiri kuwa barabara kuu ya Morogoro ndio uchumi wa nchi. Inapofungwa kwa sababu za ajali ama vurugu za wafanyabiashra wanaofanya biashara zao kwenye “road reserve”, inasitisha shughuli nyingine kutoendelea ikiwemo bandari kwani zaidi ya 80 asilimia ya makontena yanayoshushwa yanategemea barabara ya Morogoro ambayo ni kiunganishi cha mataifa ya kasikazini na kusini mwa Tanzania, maana yake tutapoteza diplomasia ya uchumi kwa nchi jirani.
Ndikilo anatumia jukwaa hilo kuwaonya wenye maduka lilipokuwepo soko la Picha ya ndege kukoma mara moja na kutopimana ubavu na serikali kwa kuwahamasisha wafanyabiashara kutokubali kuhama kwa maslahi yao binafsi kwani inajulikana kuwa walikua wanawalipa wakipanga bidhaa zao mbele ya maduka huku akiwataka wanasiasa uchwala kujiepusha na uchochezi unaolenga kuharibu mipango mizuri ya serikali.
Katika mkutano, Ndikilo anawapa nafasi wafanyabiashara kutoa ya moyoni kwa lengo la kuboresha mahusiano kati ya wafanyabiashara na watendaji wa ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ili kuongeza makusanyo ya mapato.
Rukia saidi muuzaji wa mbogamboga na Mwanahamisi Ramadhani licha ya kupongeza ziara ya Mkuu wa Mkoa kutembelea soko wanaomba kujengewa banda maalum kwa ajili ya biashara zao litakalowakinga na mvua pamoja na jua.
Saidi Utipula na Mohamedi unembwe wanaomba halmashauri kushusha kodi ya wauzaji wa matunda kutoka shilingi 10,000 inayolipwa sasa hadi 5000 huku kodi ya fremu za maduka ikishuka kutoka shilingi 8000 hadi 3000.
Kwa upande wake diwani wa Kata ya Tangini Mfalme Kabuga anawasilisha kilio cha kuharibika kwa miundombinu ya barabara hasa wakati wa mvua hali inayopelekea magari yanayoleta mazao na bidha nyingne sokoni hapo kushindwa kufika na kuwalazimu wafanyabiashara kuingia gharama ya ziada ili kuifikisha.
Katika kutatua changamoto hizo, Mhandisi Ndikilo anapaza sauti kwa kutoa maagizo yafuatayo kama sehemu ya majumuisho ya ziara yake kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha;
Mosi, watendaji wa halmashauri kukamilisha miundombinu wezeshe yote ili soko lianze kufanyakazi Choo, Umeme na Maji. Aidha, anazitaka taasisi hizo kufanya tathmini ya kutosha na kuwasilisha gharama nafuu ambazo wafanyabiashara wadogo watamudu kuzilipia.
Pili, anawaagiza wakala wa barabara nchini (TANROAD) kuendelea kuihudumia barabara inayojengwa kwa kuimwagia maji ili kupunguza vumbi huku akiwaagiza wakala wa barabara Mijini na Vijijini TARURA kuweka Kalvati sehemu zote zinazohitaji na kuhakikisha barabara zote zinafanyiwa matengenezo ili kupitika muda wote. Aidha, wakala wa usafiri wa nchi kavu na majini (LATRA) wanaelekezwa kujenga kituo cha daladala kitakachotumika kupandisha na kushusha abiria aneo la soko
Tatu ,ofisi ya mkurugenzi wa halmashauri inaagizwa kuratibu kuanzishwa kwa mnada wa gulio na mbuzi nyama choma utakaokua unafanyika kila siku ya Alhamisi ili kuhamasisha wanunuzi wa bidhaa kwenye soko hilo la msufini.
Nne, halmashauri inaekelezwa kujenge banda la wauza matunda na mbogamboga litakalo wakinga na mvua, jua huku wakikaa meza moja na wafanyabiashara kuangalia namna ya kupunguza Ushuru kutoka 10,000 unaolipwa sasa mpaka 5000 kama inafaa
Tano, wataalam wa halmashauri kufanya ukaratabati kwenye mabanda yanayovuja kujadiliana na wafanyabiashara namna ya kupungaza kodi mpaka shilingi 3000/- kutoka 8000 inayolipwa sasa kama sheria mama na sheria ndogo zinaruhusu
Sita, anamwagiza kamanda wa kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Pwani kuhakikisha magari yanayobeba abiria yanapita sokoni na kuingia stendi na sio kukatisha njia ama kushusha abiria nje ya stendi hata kama basi litakua na abiria 1 kwa hiyo ndio sheria
Ilani ya Uchaguzi wa chama cha Mapinduzi mwaka 2020-2025 inaielekza serikali kuhamasisha na kusimamia halmashauri zote nchini kuendelea kutenga, kurasimisha na kupima na kuweka miundombinu kwenye maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji na kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujishughulisha na uzalishaji mali na biashara.
Aidha, Serikali ya JPM imeendelea kuimarisha mifumo ya kisera, kitaasisi na kisheria, ikiwemo kutenga asilimia 10 ya mapato yake kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake (4%), vijana (4%) na watu wenye ulemavu (2%) ambapo kwa robo ya kwanza Julai –Oktoba halmashauri ya mji Kibaha imeshatoa zaidi ya milioni 243,000,000.00 kwa makundi hayo ili waweze kujiajiri na kujishughulisha na biashara.
Haki Zote Zimahifadhiwa