500 MILIONI KUBORESHA MIUNDOMBINU YA KITUO CHA AFYA MKOANI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imepokea kiasi cha Shilingi milioni 500,000,000.00 za miradi ya Maendeleo kutoka Serikali kuu kwa ajili ya kuimarisha na kuboresha kituo cha afya Mkoani, Halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani.
Aidha, Halmashauri ya Mji Kibaha ni Miongoni mwa Halmashauri zilizopata fedha hizo ili ziweze kuboresha miundombinu yake itayokwenda sambamba na utoaji wa huduma bora inayoendana na mahitaji halisi ya wananchi kwa sasa.
Akiwasilisha mbele ya madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na ugavi wa Halmashauri ya mji Kibaha Alphonce Temba alisema uboreshaji huu ni malengo mahususi ya Mpango Mkakati wa nne wa Sekta ya afya (HSSP-IV) ambapo utaratibu wote wa manunuzi utatumia ‘force Account’ ili kupunguza gharama za ujenzi na muda ingawa ubora wa majengo yanayojengwa utazingatiwa.
Kwa upande wake mkurugenzi wa Mji Kibaha Bi. Jenifa Omolo alisema kuwa Utaratibu huu kwa Halmashauri ya Mji Kibaha unaonekana kama mpya ingawa Halmashauri nyingine zimekuwa zikiutumia na umeonekana kuwa na tija.
“Mheshimiwa Mwenyekiti utaratibu huu wa manunuzi ni kwa mujibu wa ibara ya 17 ya kanuni ya Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2013, uzuri wake ni kupunguza gharama na kuongeza ubora wa ujenzi husika kwani badala ya kutumia mkandarasi ambaye huwa na mchakato mrefu wa manunuzi ya kawaida, sasa unaweza kutumia mafundi wa kawaida “local fund” na manunuzi yote unakwenda mwenyewe dukani na unanunua bei ya soko kama sementi ni 12,500/-unalipa hiyo lakini lazima ulipe kodi ya serikali kwa kupewa risiti ya mashine ya kieletroniki (EFD)” alisema
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Leonard Mlowe aliishukuru serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuikumbuka Kibaha na kuwataka wataalamu kuzingatia utaratibu, kanuni, sheria. miongozo, weledi na maadili ya utumishi wa umma wakati wa utekelezaji.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dr. Tulitweni Mwinuka alisema kuwa fedha hizi zitatumika kujenga jengo la upasuaji, Wodi ya watoto na akina Mama, Jengo la Xray, Sehemu ya kufulia na nyumba ya mtumishi
Haki Zote Zimahifadhiwa