Watendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Wafanya Mafunzo ya Ukusanyaji Mapato na Utunzaji wa Mazingira Jijini Mbeya
Mbeya – Julai 8, 2025
Watendaji kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wameanza rasmi mafunzo maalum kuhusu ukusanyaji wa mapato katika vyanzo vya leseni ya makazi, utunzaji wa mazingira, pamoja na utoaji wa mikopo kwa makundi maalum ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mafunzo hayo yanafanyika katika ukumbi wa Jiji la Mbeya, yakilenga kuboresha utoaji huduma na kuongeza mapato ya halmashauri.
Mafunzo hayo yametolewa na wataalamu kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya akiwemo Bw. Deus Muhoja, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, pamoja na Bw. Ramadhani Likwina, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Udhibiti Taka Ngumu na Usafishaji.
Wataalamu hao wameeleza mbinu mbalimbali zinazotumika jijini Mbeya katika ukusanyaji wa taka na kudumisha usafi wa mazingira.
Katika ziara ya mafunzo ya vitendo iliyofanyika ofisini ya Kata ya Luanda na dampo la Nsalaga, watendaji wa Kibaha walijionea namna Jiji la Mbeya linavyotumia taka ngumu kama kichocheo cha maendeleo.
Imeelezwa kuwa watendaji wa kata jijini Mbeya wamepewa dhamana ya kusimamia taka hizo, jambo ambalo limewawezesha kutatua changamoto mbalimbali katika kata zao ikiwemo kuhakikisha Jiji lao kinakuwa safi muda wote.
Kata ya Luanda imekuwa mfano wa kuigwa kwa namna ilivyofanikiwa kujenga Ofisi bora ya kata na kusaidia miradi ya maendeleo kupitia mapato ya taka, ikiwa ni pamoja na kununua bati, kulipa walinzi na vibarua kutokana na chanzo Cha taka.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha amesema kuwa lengo kuu la ziara hiyo ni kujifunza mbinu bora za kuongeza mapato na kuziboresha huduma za Halmashauri ya Manspaa Kibaha.
Kwa upande wao, watendaji wa Kibaha wameahidi kutumia ujuzi walioupata kuboresha ukusanyaji wa mapato na huduma kwa wananchi.
Ziara hiyo itaendelea kesho katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma kwa lengo la kuendeleza mafunzo hayo kwa vitendo na kujifunza kutoka kwa halmashauri nyingine zenye mafanikio makubwa.
Haki Zote Zimahifadhiwa