Na Byarugaba Innocent,Pwani
Wajumbe wa menejimenti ya wataalam halmashauri ya Mji Kibaha inayowaunganisha Wakuu wa Idara na vitengo wametembelea Mradi wa ujenzi wa Majengo Saba unaoendelea kwenye hospitali ya Wilaya Lulanzi yanayogharimu Bilioni 1.3 mpaka kukamilika.
Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan imeidhinisha kiasi kikubwa cha fedha ili kupanua wigo wa utoaji wa huduma za kitabibu kwa wananchi wake sambamba na kuwapunguzia safari ndefu za kufuata huduma hizo kwenye maeneo mengine ikiwemo hospitali ya Tumbi na hospitali ya Muhimbili-Mloganzila.
Katibu wa afya Prosper Juma ameyataja Majengo yanayojengwa kuwa ni wodi ya Wanaume,wanawake na watoto zitakazogharimu milioni 500 na Sasa zipo hatua ya umaliziaji.Aidha,majengo matatu ya upasuaji na jengo la kuhifadhia maiti yatagharimu milioni 800 na Sasa yapo hatua ya jamvi na Kupandisha Kuta.
Mganga mfawidhi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Dr.Sabinusi Ndunguru ameeleza kuwa changamoto sugu ya kukosekana kwa Maji hivyo kama mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira (DAWASA) wataendelea kutokuwa na ushirikiano Mradi hautakamilika kwa wakati hivyo kuwa kero kwa wananchi badala ya neema.
"DAWASA tumewapelekea hoja ya kukosa Maji muda mrefu lakini hatuoni mwitikio wao,tumewafuata Ofisini kuwakumbusha mara kwa mara bado hatupati matumaini ya Maji,nahofia Mradi huu kukamilika kwa kuchelewa"amesema Dr.Ndunguru.
Aidha,amesema kuwa wakati wa kuanza ujenzi wa hospitali hiyo.... halmashauri kwa gharama za Mapato ya ndani kiasi cha zaidi ya milioni 20 ilinunua bomba lake na kuliunganisha kwenye bomba kubwa umbali wa takribani Kilomita 2.5 hata hivyo DAWASA walilichepusha na kuwaunganishia wananchi na kufifisha Kasi ya Maji kufika hospitalini.
Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Kibaha John Alexander Kuna zaidi ya Majengo matano wakandarasi wamesimama kutokana na ukosefu wa Maji na kwamba hali hiyo ni kiashiria cha kutokamilika kwa wakati
Mhandisi Alexander ameongeza kuwa mpaka sasa zaidi ya milioni 1.5 zimetumika kununua Maji ya boza kama sehemu ya kwenda na kasi ya Ujenzi unatakiwa kutamatishwa Oktoba 15 2022 lakini gharama ni kubwa na kama wataendelea wataathirika kwenye bajeti kwani kwenye fedha ya Serikali hakuna fungu la ununuzi wa Maji .
Hata hivyo,katika harakati za kukwamua Mradi kukwama menejimenti ilikwenda Ofisi za DAWASA Kibaha na kukutana na mwanasheria wao Humphrey Massawe aliyekiri uwepo wa tatizo hilo na kuahidi kulifikisha kwenye mamlaka za juu kwa utekelezaji.
Mpaka sasa jumla ya bilioni 3.39 zimeshatolewa na Serikali kwa ajili ya hospitali ya Wilaya Lulanzi.
Haki Zote Zimahifadhiwa