"MKUU WA WILAYA YA KIBAHA AFUNGUA RASMI MAFUNZO YA SIKU TATU KWA MADIWANI WA PWANI
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kwa kushirikiana na Chuo Cha serikali za Mitaa Hombolo (LGTI) inaendesha mafunzo ya siku tatu kwa Waheshimiwa Madiwani kutoka wilaya tatu za Mkoa wa Pwani ambazo ni Kibaha, Rufiji na Bagamoyo, kwa lengo la kuwajengea uwezo katika utekelezaji wa majukumu yao ya udiwani.
Mafunzo hayo yanafanyika katika Ukumbi wa Destiny, Kwa Mathias, Manispaa ya Kibaha, yakilenga kuwajengea madiwani uwezo katika masuala ya uongozi, usimamizi wa rasilimali watu pamoja na utawala bora.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mheshimiwa Nickson Simon, amewataka madiwani kushiriki mafunzo hayo kwa umakini na kuyatumia kama fursa ya kuongeza maarifa yatakayowasaidia kuwahudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
Mheshimiwa Simon amesisitiza umuhimu wa matumizi ya lugha yenye hekima, maadili na busara katika vikao na maamuzi ya kiuongozi, akieleza kuwa chuki, hasira na wivu havijengi bali huvunja mshikamano na kuchelewesha maendeleo ya jamii.
Aidha, amebainisha kuwa mabadiliko ya kweli katika jamii yanahitaji viongozi kuwa na mawasiliano mazuri na wananchi wao, sambamba na kuwa tayari kujifunza kupitia uzoefu wa wengine na mazingira tofauti.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya amewataka madiwani kuwa tayari kupokea ukosoaji na kutambua kuwa ukosoaji ni sehemu ya kuboresha utendaji kazi, siyo shambulio binafsi.
“Wakati wa kutoa hoja au kukosoa, hakikisheni mnakosoa mawazo au utendaji na siyo kumshambulia mtu binafsi. Ni muhimu kila mmoja kutunza utu wa mwenzake,” amesisitiza Mheshimiwa Simon.
Vilevile, amewahimiza madiwani kufanya kazi kwa mshikamano na umoja, akieleza kuwa umoja wao ndio msingi wa kuleta maendeleo chanya kwa wananchi wanaowawakilisha. Amehitimisha kwa kutoa wito wa kuweka pembeni tofauti binafsi na kushirikiana kwa maslahi mapana ya umma.
Haki Zote Zimahifadhiwa