DC KIBAHA ABARIKI WAZAZI KUCHANGIA CHAKULA SHULENI
Na.Innocent Byarugaba, Kibaha
Mkuu wa wilaya ya kibaha Mhe.Sara Msafiri amewataka wazazi na walezi wa watoto wanaosoma shule za msingi kwenye halmashauri ya Mji Kibaha kuwachangia chakula shuleni ili kuinua kiwango cha elimu.
Hayo ameyaeleza mwanzoni mwa wiki kwenye halfa ya uzinduzi wa kampeni ya utoaji chakula shuleni iliyofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Kongowe.
Msafiri alibainisha kuwa kutokana na ukokotoaji wa wataalam wa idara ya elimu imeonyesha kuwa kila mwanafunzi anakula kilogram 25 za unga/mchele na maharage kilogram 10 kwa mwaka mzima kitu ambacho wazazi wanaweza kumudu kuchangia iwapo watajinyima kununua vijora na mambo mengine yasiyokuwa na tija.
Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za jamii ambaye pia ni diwani wa kata ya Mailimoja Mhe. Ramadhani Lutambi alisema umefika wakati muafaka kwa shule za Halmashauri ya Mji Kibaha kuanza utaratibu wa kuchangia chakula shuleni ili watoto wapate chakula kuinua kiwango cha elimu kwani si jambo geni maeneo mengine ikiwemo mikoa ya kaskazini huo utaratibu ni kawaida na wanafunzi wameonekana wakifanya vizuri kitaalumaDiwani wa Kata ya Kongowe Mhe. Hamisi Shomari aliwaomba wazazi wa Kongowe kuiga mfano wa shule ya Mwambisi ambayo miaka ya nyuma ilikuwa na hali mbaya kitaaluma lakini baada ya kuanzishwa utaratibu wa wanafunzi kula chakula shuleni sasa imeimarika na kushika nafasi ya kwanza kimkoa mwaka 2020 na mwaka 2021 watoto wote wamefaulu kuingia kidato cha kwanza huku ikishika nafasi ya nne kimkoa.
Afisa Elimu Msingi Bernadina Kahabuka kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha, alitoa rai kwa wazazi kuupokea mpango huo na kuutekeleza kwani kwa kufanya hivyo kutaimarisha afya za watoto, kuongeza ufaulu na kuinyanyua halmashauri nzima kwenye ufaulu.
Halfa hiyo kando ya kamati ya ulinzi na usalama ilihudhuriwa na Wahe. Madiwani, Maafisa Elimu kata, Walimu wakuu wa shule zote za msingi, Wajumbe wa Serikali na Wananchi wengine
Haki Zote Zimahifadhiwa