Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amefanya ziara ya kikazi Kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha kutembelea kampuni za Organia na Mkuza Chicks za Ufugaji Kuku na utotoleshaji wa Vifaranga vya Kuku wa Mayai na Nyama ili kuona Maendeleo ya sekta hiyo.
Akiwasilisha taarifa ya kampuni ya Organia,Ofisa Mahusiano Secky Ngwilizi amezitaja changamoto kuwa ni upatikanaji wa malighafi za utengenezaji wa Chakula kama Soya na Mahindi na hata yakipatikana bei ni kubwa toka kwa wakulima.
Ngwilizi aliongeza kuwa changamoto nyingine ni uingizaji wa Vifaranga kutoka nchi jirani kwa njia ya Magendo na kwamba kando ya kuhujumu uchumi wa wanaharibu Soko la Vifaranga vya hapa nchini kwa kuuza bei nafuu isiyoendana na gharama za uendeshaji
"Mheshimiwa Naibu Waziri,Kampuni yetu inafuata sheria zote za uwekezaji,inalipa Kodi,Vibali vyote vya uwekezaji vipo,watumishi 126 wameajiriwa na wanalipwa mishahara,haiwezekani Vifaranga vikauzwa bei sawa na kampuni zinazoingiza Vifaranga toka nje kwa njia za Magendo"
Aidha, Ngwilizi aliongeza kuwa Soko la Vifaranga halilidhishi na imekuwa changamoto ya muda mrefu akitolea uhalisia wa boksi 250 za Vifaranga vilivyozalishwa usiku wa kuamkia Julai 12,2022 wamekosa Soko na hakuna kwa kuwapeleka zaidi ya kuwasubiri wafe kifo cha Kawaida kutokana na kukosekana kwa wateja
Akitoa kauli ya Serikali Naibu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewaelekeza wataalam wa sekta ya Ufugaji wa Kuku kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na kwamba Vibali vya uingizaji na uagizaji wa Vifaranga vitolewe pindi vinapokosekana nchini.
Aidha Ulega ametoa rai kwa wafugaji wote nchini takribani asilimia 60 ya kaya kuwasilisha changamoto za Vifaranga vinavyozalishwa nchini ili zitafutiwe utatuzi na kwamba kununua toka uje ni kukosa uzalendo na kuangamiza uchumi wa Taifa letu.
Kwa upande wake Meneja uendeshaji wa Kampuni ya Mkuza Chicks Bi.Florence Maximambali ametoa wito kwa Serikali kuweka mkakati mahsusi kuhakikisha wawekezaji wazawa wanalindwa kwani sekta ya Ufugaji wa Kuku inachangia uchumi wa nchi,kipato cha Kaya na kuimarisha afya ya walaji kwa kutoa protini lishe.
Naibu Ulega alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuhamasisha uwekezaji nchini na kwamba kazi yetu Watanzania ni kulinda uwekezaji uliopo kwani ni chanzo cha haraka cha ajira.
Ulega alifuatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri, Mkurugenzi wa Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde pamoja na wataalam wa mifuko kutoka Wizarani,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani na Halmashauri ya Mji Kibaha.
Haki Zote Zimahifadhiwa