Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha Yakamilisha Zoezi la Upimaji wa Viwanja Kata ya Viziwaziwa
Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imekamilisha rasmi kazi ya kuwatambua wananchi, kupanga maeneo, kupima viwanja na kukabidhi ramani za upimaji katika Kata ya Viziwaziwa.
Zoezi hilo limehitimishwa kwa mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Mtendaji wa Kata ya Viziwaziwa Manispaa ya Kibaha.
Mgeni rasmi katika mkutano ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, ambaye amewataka wananchi kutimiza wajibu wao kwa kulipia viwanja walivyopimiwa na Serikali ili waweze kupata hati miliki halali.

Ameongeza kuwa Serikali imekamilisha majukumu yake ya kupanga maeneo na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi, hivyo ni jukumu la wananchi sasa kushiriki kwa kulipia viwanja hivyo kwa mujibu wa taratibu za kisheria.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, amesema kuwa jumla ya viwanja 761 vimepimwa kwa kuzingatia taratibu zote za kitaalamu na tayari ramani zake zimekamilika. Ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kulipia viwanja hivyo ili waweze kumilikishwa kihalali na kuepuka migogoro ya ardhi.
Aidha Kwa kuwaletea huduma karibu wataalamu wa Ardhi na fedha watakuwa wanatoa huduma hizo katika Ofisi ya Mtendaji Kata ya Viziwaziwa na kuwataka Wananchi kuchangamkia fursa ya kuletewa huduma karibu.
Wananchi wa Kata ya Viziwaziwa wameeleza furaha yao kwa hatua hiyo ya Serikali, wakimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa juhudi zake katika kutatua changamoto za muda mrefu na kuleta utulivu katika jamii. Wamesema kuwa hatua hiyo imewafanya waishi kwa amani na kuwa na matumaini makubwa ya maendeleo na Serikali Kwa ujumla.
Haki Zote Zimahifadhiwa