HALMASHAURI YA MJI KIBAHA YAKUSANYA MAPATO YA NDANI ASILIMIA 102
Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Halmashauri ya Mji Kibaha imeweza kukusanya Mapato ya ndani kwenye vyanzo vyake kiasi cha shilingi 4,834,233,839 sawa na asilimia 102 ukilinganisha na shilingi 4,591,068,424 zilizokadiriwa kukusanywa katika Mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni ongezeko la shilingi 243,165,415.
Akiwasilisha taarifa ya Mapato na matumizi kwenye kikao cha baraza la Madiwani robo ya nne kilichoketi kilichoketi mwishoni mwa wiki kwenye Ukumbi wa halmashauri hiyo,Mheshimiwa Selina Msenga ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ameeleza kuwa kwa Mwaka wa fedha 2021/2022 ilikadiriwa kukusanya jumla ya shilingi 39,436,683,192 kutokana na Mapato yatokanayo na ruzuku,Mapato ya ndani pamoja na washiriki wengine wa maendeleo.
Aidha, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mheshimiwa Mussa Ndomba amewapongeza Waheshimiwa Madiwani kwa ushirikiano wao na Wakuu wa idara na Vitengo kwenye suala muhimu la kukusanya Mapato na kufikia lengo walilojiwekea kwa kishindo pamoja na malengo ya Serikali inayoongozwa na Rais wa awamu ya Sita Mhe.Samia Suluhu Hassan.
"Waheshimiwa Madiwani wenzangu nawapongeza kwa kazi kubwa ya kusimamia ukusanyaji wa Mapato.Aidha,nawapongeza Sana Kitengo cha fedha kwa uratibu mzuri,kipekee nampongeza Mkurugenzi pamoja na timu yake ya Wakuu wa Idara na vitengo kwa kushiriki vema kwenye ukusanyaji wa Mapato.Hata hivyo kwa Mwaka wa fedha 2022/2023 Waheshimiwa Madiwani tutapanua wigo,hatutaangalia makusanyo pekee.Tutaangalia pia matumizi ya fedha zinazokusanywa"alisema Mhe.Ndomba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde amebanisha vyanzo vikuu vya Mapato ya ndani kuwa ni Kodi ya huduma ambayo imechangia shilingi 1,419,956,677,Mauzo ya Viwanja shilingi 1,427,677,376,ushuru wa Stendi shilingi 601,058,300,leseni za biashara shilingi 314,020,262 na ushuru wa mchanga shilingi 219,321,000 na kwamba vyanzo hivyo ni sawa na asilimia 20 inayochangia asilimia 80 ya Mapato yote ya halmashauri.
Hata hivyo amebainisha kuwa lengo la Serikali ni kukusanya Mapato halali na kuziba mianya ya ufujaji ili yatumike kutolea huduma kwa wananchi hivyo wamejipanga kutoa Elimu ya Kodi kwa wananchi ili kuwapa hamasa ya kutoa bila shuruti ikiwa ni pamoja na kuongeza nguvu kwenye vyanzo vingine ambavyo havifanyi vizuri kama vile kwenye Maeneo ya Vibali vya ujenzi,ushuru wa machinjio,ushuru wa Malazi na vyanzo vingine ili kuongeza Mapato yatakayotumika kuwaletea Maendeleo wananchi wenyewe.
Ikumbukwe kuwa Serikali yoyote duniani pamoja na Mapato mengine yatokanayo na rasilimali zake zilizomo,bado chanzo kingine huwa ni Kodi na tozo mbalimbali,hata hivyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ameagiza kuwa tozo na ushuru mbalimbali wanazo tozwa Wananchi na wafanyabiashara zitozwe kisheria na zisiwe kero kwao zaidi ziwe rafiki.
Haki Zote Zimahifadhiwa