Na Byarugaba Innocent, Kibaha
Kando ya siku Saba za nyongeza zilizotangazwa na Kamisaa wa sensa ya watu na Makazi nchini Anna Semamba Makinda ili kuhitimisha zoezi hilo, halmashauri ya Mji Kibaha mpaka kufikia Agosti 29,2022 imevuka lengo la uandikishaji kwa kufikisha kaya 66,011 sawa na asilimia 146.12 dhidi ya kaya 45,176 zilizokadiriwa awali.
Halmashauri ya Mji Kibaha yenye jumla ya Kata 14 hakuna iliyohesabu kaya pungufu ya asilimia 100 huku kata kinara ikiwa ni Sofu iliyokadiriwa kaya 1064 na Sasa imefikisha kaya 1996 sawa na 187.59 asilimia na Kata ya Viziwaziwa yenye asilimia 107.25 ikihesabu kaya 1583 kati ya 1476 zilizokadiriwa.
Mratibu wa sensa ya watu na Makazi wa halmashauri ya Mji Kibaha Wambura Yamo amesema hamasa kubwa na shirikishi iliyofanywa ya kuwahamasisha wananchi kushiriki Zoezi la Sensa ya watu na Makazi kuanzia ngazi ya Taifa mpaka kwenye Vitongoji, Vijiji na Mitaa imekuwa Chachu na kuleta ari na mwitikio na ushirikiano chanya kati ya wananchi na Makarani wa sensa hivyo tutegemee kupata idadi kubwa ya Watanzania itayoleta urahisi kwa Serikali kupanga Mipango bora ya utoaji huduma kwa faida ya nchi na wananchi wenyewe.
Wambura kipekee amempongeza na kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kiongozi kinara wa uhamasishaji wa Watanzania kuhesabiwa kwani amekuwa akitoa ujumbe mfupi kila siku hali iliyowamotisha wananchi na kuitikia wito wa kuhesabiwa ili kuunga mkono juhudi za Serikali yao katika kupanga ama kuboresha huduma zote muhimu ikiwemo kiuchumi,Kijamii ,kidemographia na kiutamaduni.
"Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mheshimiwa Sara Msafiri na Kamati yake ya Usalama ameshiriki kikamilifu kwenye zoezi hili la Sensa tangu siku ya mwanzo mpaka leo bila kuchoka,ameonesha mfano wa kuigwa kwa wananchi kwani kila palipotokea changamoto alifika kwa wakati kuitatua,anasitahili pongezi "amesema Wambura
Kwa upande wake Getruda Kalenzi amesema kutokana na hamasa kubwa iliyofanywa Mwaka huu alijawa na shauku ya kuhesabiwa.Amesema kuwa ingawa maswali yalikuwa mengi lakini yalikuwa mazuri kwani yalisheheni taarifa muhimu tena za Msingi zinazotakiwa kwenye upangaji wa Mipango ya maendeleo ya Taifa.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde mbali na kuwapongeza viongozi wa Kitaifa kwa maandalizi mazuri ya Sensa ya watu na Makazi 2022, amewashukuru viongozi wa dini wa madhehebu yote, Watendaji wa Kata mpaka Vitongoji na Mabalozi wa nyumba kumi kwa ushirikiano na uzalendo waliouonesha kufanikisha suala hili nyeti kwa Mipango ya Taifa na wananchi wake.
Haki Zote Zimahifadhiwa