JESHI LA ZIMAMOTO NA UOKOAJI PWANI WAADHIMISHA SIKU YA KUPUNGUZA MAJANGA DUNIANI
Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Pwani, kwa kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu, leo tarehe 13 Oktoba 2025, wameadhimisha Siku ya Kupunguza Majanga Duniani kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii.
Akizungumza katika tukio hilo, Kamanda wa Zimamoto mkoa wa Pwani, Jenifa Shirima, amesema kuwa wameamua kushirikiana na Shirika la Msalaba Mwekundu ili kutoa elimu na kufanya kazi za kijamii, kama njia ya kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuchukua tahadhari na kupunguza athari za majanga.
“Kupitia maadhimisho haya, tunalenga kutoa funzo kwa jamii ili iweze kujifunza namna ya kujikinga na kuchukua hatua za mapema katika kupunguza majanga mbalimbali,” alisema Kamanda Shirima.
Aidha, mbali na kutoa elimu kwa wananchi, maadhimisho hayo yalihusisha shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo usafi wa mazingira, uchangiaji wa damu, pamoja na kugawa bidhaa kama sabuni, taulo za watoto na vifaa vya usafi kwa wahitaji.
Kwa upande wake, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha, Bwana Amor Mohamed, ametoa shukrani kwa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kuwakumbuka na kuwatembelea, akisema hatua hiyo inaonesha moyo wa huruma na kujitolea kwa ajili ya jamii.
Haki Zote Zimahifadhiwa