Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Bi Pili Mnyema, ametoa wito kwa wakulima wa maeneo ya mijini kutumia teknolojia ya kisasa katika kilimo na ufugaji ili kuongeza tija na kipato chao.
Akizungumza wakati akiwa Mgeni Rasmi wa Maonesho ya Nanenane katika Banda la Halmashauri ya Manispaa Kibaha, Bi Mnyema amewahimiza wakulima wa mjini kutumia mbinu bora za kilimo cha kisasa ikiwemo matumizi ya nyavu za mazao yanayotambaa, pamoja na kufuga mifugo kwa njia za kitaalamu katika maeneo ya mijini yenye nafasi ndogo.
“Tunaamini kuwa kilimo cha mjini ni mkombozi mkubwa wa kipato kwa wananchi. Ni muhimu kutumia teknolojia na maarifa ya kisasa ili kuzalisha zaidi kwa tija hata katika maeneo madogo,” alisema Bi Mnyema.
Aidha, Katibu Tawala huyo ameipongeza Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha kwa hatua ya kuhimiza matumizi ya teknolojia katika kilimo na ufugaji wa kisasa, na kueleza kuwa juhudi hizo zinapaswa kuungwa mkono na wakulima wote wa mjini.
Amesisitiza kuwa wakulima na wafugaji wanapaswa kufuata maelekezo ya kitaalamu kutoka kwa maafisa ugani ili kuweza kuzalisha kwa ufanisi na kuhakikisha usalama wa chakula katika maeneo ya mijini.
“Maendeleo ya sekta ya kilimo mijini yanategemea kwa kiasi kikubwa ushirikiano wa wananchi na wataalamu. Tufuate ushauri ili tufanikiwe,” aliongeza.
Haki Zote Zimahifadhiwa