Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya imeanza zoezi la Kitaifa la kutoa chanjo ya matone ya kutokomeza Polio kwa watoto wote wenye umri wa chini ya miaka mitano kuanzia Septemba 1,2022 kukiwa na lengo la kuwafikia watoto 12,386,854 Kitaifa katika awamu hii ya tatu.
Aidha,Halmashauri ya Mji Kibaha ambayo imepewa dozi 40,000 inatarajia kutoa chanjo hiyo kwa watoto wasiopungua 38748 kwa awamu hii kwenye Kata 14 na Mitaa 73 inayounda Halmashauri hiyo ambapo tayari watoto 11,347 sawa na asilimia 30.3 wamepata chanjo siku ya kwanza
Awali akiwasilisha taarifa ya mikakati ya kufanikisha zoezi hilo kwenye kamati ya PHC,Mratibu wa chanjo Halmashauri ya Mji Kibaha Hope Rutatina amesema jumla ya timu 69 zenye wataalam watatu kila moja zimeundwa kwa ajili ya kufanikisha na kwamba zitatembea nyumba kwa nyumba ili kuwafikia walengwa.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri Dkt.Tulitwen Mwinuka ametoa rai kwa wazazi na walezi wote kuhamasika na kuchangamkia fursa hiyo inayotolewa bure ili kuepuka gharama kubwa za kumtibia mgonjwa wa polio kwani madhara yake ni Makubwa.
"Ndugu wajumbe wa PHC niwaombe tushirikiane kuwahamasisha wananchi kutoa ushirikiano kwa watoa huduma ya chanjo,chanjo hii ni salama na imegharamiwa na Serikali.Tuwape Elimu kuwa madhara ya ugonjwa wa Polio ni Makubwa ikiwa ni pamoja na ulemavu wa viungo ambavyo matibabu yake yanahitaji fedha nyingi.Chanjo zipo nyingi na mara zote zimekuwa na mafanikio ya kuzuia maradhi" amesema Dkt.Mwinuka
Dkt.Mwinuka ameongeza kuwa chanjo hiyo inatolewa kwa kila Mtoto mwenye umri wa chini ya miaka mitano hata kama alishawahi kupata awali kwani ugonjwa wa Polio ni hatari hivyo amewasihi Wazazi na walezi kuondoa shaka kwani iwapo Mtoto atapata madhara Serikali itagharamia matibabu yake.
Kupitia taarifa kwa Umma iliyosainiwa na Waziri wa Afya nchini Mheshimiwa Ummy Mwalimu Agosti 30,2022 imeonyesha maelekezo ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kila nchi kufanya kampeni ya kutoa chanjo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kwa awamu nne mfululizo ili aweze kupata Kinga kamili endapo kutatokea mlipuko au tishio la ugonjwa wa Polio nchini mwake.
Taarifa za kitabibu zinaonesha kuwa chanzo cha ugonjwa wa Polio husababishwa na kirusi ambacho huambukizwa kutoka kwa mtu aliyeathirika kwenda kwa mtu mwingine kwa kula au kunywa kitu kilichochafuliwa na kinyesi chenye virusi vya Polio.
Haki Zote Zimahifadhiwa