Katika jitihada za kuinua uchumi wa kaya na kuimarisha lishe bora kwa wananchi, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha inaendelea kutoa elimu ya kilimo cha mbogamboga katika maeneo ya mijini, hususani kupitia Maonesho ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere mkoani Morogoro, Kanda ya Mashariki.
Akizungumza katika banda la Manispaa ya Kibaha, Afisa Kilimo wa Manispaa hiyo, Joseph Njau, amewahamasisha wananchi kutembelea banda hilo ili kupata mafunzo ya kilimo cha mbogamboga, ambacho kimekuwa na manufaa makubwa kwa wakazi wa mijini.
“Tunatoa elimu ya kilimo cha mbogamboga kwa njia nyepesi na ya vitendo. Wananchi wanajifunza jinsi ya kutumia maeneo madogo kama vile viwanja vya nyumba zao kuzalisha chakula kwa tija na kipato,” alisema Njau.
Kwa mujibu wa Afisa huyo, faida kuu za kilimo cha mbogamboga ni pamoja na:
Kuimarisha afya kwa kuwapatia watu lishe bora yenye virutubisho muhimu,
Chanzo cha kipato kwa wakulima na vijana wanaojishughulisha kilimo,
Kinga dhidi ya magonjwa mbalimbali kutokana na ulaji wa mbogamboga zenye virutubisho muhimu,
Kilimo Cha mjini kinatumia eneo dogo huku kizalisha kwa tija kubwa.
Ameongeza kuwa kilimo cha mjini (urban farming) kimekuwa suluhisho la uhaba wa chakula na ajira katika maeneo ya mijini, na kuwataka wananchi kuiga mfano huo na kuanza kulima mbogamboga hata kwa kutumia vifaa rahisi kama mapipa, viroba, mifuko au vichanja.
"Wananchi wasisite kutembelea banda letu la Manispaa ya Kibaha katika maonesho ya Nanenane ili wajifunze na waanze kilimo hata nyumbani kwao. Hili ni jambo linalowezekana na lenye faida ya haraka," alihimiza Njau.
Maonesho ya Nanenane Kanda ya Mashariki yanaendelea kuvutia wakulima kutoka maeneo mbalimbali nchini, yakitoa elimu na teknolojia bunifu zinazosaidia kuimarisha kilimo katika mazingira ya sasa.
Haki Zote Zimahifadhiwa