Kibaha, Julai 25, 2025 – Kiwanda cha XINGHAO GROUP COMPANY LTD ( LULU CEMENT) tarehe 25/07/2025 kimekabidhi madawati 200 yenye thamani ya shilingi milioni 33, pamoja na shilingi milioni 3 kwa ajili ya ununuzi wa fenicha za walimu katika Shule ya Msingi Misugusugu, iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha, mkoani Pwani msaada wenye thamani ya TSH milioni 36.
Msaada huo umetolewa kwa lengo la kutatua changamoto ya uhaba wa madawati na samani kwa walimu, ili kuimarisha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji shuleni hapo.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Meneja wa kiwanda hicho, Bw. Wan Jianguo, amesema kuwa kiwanda hicho kmeanza shughuli zake katika eneo hilo mwaka jana, na walipofanya ziara shuleni hapo walibaini changamoto mbalimbali, ikiwemo uhaba wa madawati licha ya serikali kuwa imejenga miundombinu bora.
“Tumeona ni wajibu wetu kama wawekezaji kushiriki kuboresha mazingira ya elimu kwa watoto wetu. Serikali imefanya kazi kubwa ya kujenga miundombinu, sasa sisi tunachangia kuiwezesha shule kuwa na vifaa vya msingi vya kujifunzia,” alisema Bw. Jianguo.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Mkuu wa Divisheni ya Elimu ya Awali na Msingi, Mwl.Theresia Kyara, akipokea msaada huo amewashukuru wawekezaji wa Xinghao Group Company Ltd kwa moyo wa uzalendo na mchango wao katika maendeleo ya elimu.
“Msaada huu utakwenda moja kwa moja kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi na mazingira ya kufundishia kwa walimu wetu. Tunaahidi kuwa vifaa hivi vitatumika kikamilifu kama ilivyokusudiwa,” alisema Mwl. Kyara.
Aidha, aliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji nchini, jambo ambalo limewezesha wawekezaji wengi kushiriki katika maendeleo ya jamii.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa eneo la Misugusugu walioshiriki hafla hiyo wamelwapongeza wawekezaji hao kwa msaada huo na kuahidi kushirikiana nao katika kuendelea kutatua changamoto nyingine zinazoikabili shule hiyo.
“Huu ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya wawekezaji na jamii. Tunaahidi kuwa walinzi wa miundombinu na vifaa hivi,” alisema mmoja wa wazazi waliokuwepo katika hafla hiyo.
Haki Zote Zimahifadhiwa