MADIWANI KIBAHA MJINI WAPATA MBINU MPYA ZA UKUSANYAJI MAPATO
Na Innocent Byarugaba, Kibaha
Madiwani wa halmashauri ya Mji Kibaha wamepata mafunzo ya mbinu bora za ukusanyaji wa mapato ya ndani, utekelezaji wa miradi kupitia mfumo wa force account na maandalizi na utekelezaji wa mpango wa bajeti katika kikaokazi cha siku moja kilichofanyika kwenye ukumbi wa halmashauri hiyo mwishoni mwa wiki kwa lengo la kuimarisha makusanyo yatakayowesha kutoa huduma stahiki kwa wananchi na matumizi sahihi ya rasilimali fedha.
Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya Mji Kibaha Mhe.Selina Wilson Msenga amesema kuwa kuwa mafunzo hayo muhimu yametolewa wakati sahihi na kutoa rai kwa Wahe.Madiwani kuyazingatia ili yalete tija.
Aidha, Mwenyekiti wa Halmashauri Mhe. Mussa Ndomba amesema kuwa mada zote tatu ni muhimu sana ingawa zimekuwa zikitekelezwa kwa nyakati tofauti.
“Hizi mada zimekuja kwa wakati wahe. Madiwani. Tuzisikilize kwa makini hasa ukizingatia kuwa mwaka mpya wa fedha unaoanza Julai, 2022 tutaanza kutekeleza bajeti mpya” amesema na kuongeza.
Vicent Mirambo akiwasilisha mada ya ukusanyaji wa mapato amewashauri Wahe.Madiwani kujua taratibu,vishiria na udhibiti wa mapato yanayokusanywa kwani serikali imeweka utaratibu rafiki wa kukusa nya kwa njia ya kieletroniki ili kuziba mianya ya upotevu lakini bado changamoto hiyo ipo.
Mirambo ameeleza kuwa mapato ya ndani ya halmashauri hukusanywa kutokana na makadirio yaliyowekwa na uwezo wa vyanzo vilivyopo ingawa mara nyingine makadirio huwa madogo ambayo hupelekea makusanyo kuwa makubwa.
“Wahe. Madiwani kukusanya sana ni vizuri, lakini sio sifa njema kwani hicho ni kiashiria kuwa makadirio yenu mlipanga kidogo” amesema
Aidha ameshauri kuwa na upangaji na makadirio mazuri yatakayowezesha kutekeleza vipaumbele vilivyopo ambapo takwimu za vyanzo husika ni muhimu kuwepo ili kufanya makusanyo kuwa halisia
Hali kadhalika amewakumbusha kuwa uandaaji wa makadirio ya mapato ya ndani katika halmashauri hufanyika kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo ya serikali huku akikumbusha baadhi ya sheria zinazoongoza kuwa ni Sheria ya fedha za Mamlaka ya Serikali za Mitaa sura 290 (1982) na mapitio ya 2019, Memoranda ya fedha za Mamlaka za Serikali za Mitaa 2009; Sheria ya bajeti (2015), Mwongozo wa bajeti unaotolewa kila mwaka na Wizara ya Fedha na Mipango; Sheria ndogo za Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mpango mkakati wa Halmashauri na sera za Kitaifa zinazoongoza sekta mbalimbali
Mirambo ameongeza kuwa kando ya uwepo wa kanzi data ili kufikia malengo la makadirio ni vema kutambua uwezo wa kila chanzo, kutambua vyanzo vichache vinavyobeba mapato makubwa ili kuviwekea msisitizo, kuwa na mikakati sahihi ya kukusanya, kuwianisha bajeti husika na kuweka ukomo wa bajeti ingawa Wizara husika inaweza kuongeza au kupunguza kadri itakavyoona uhalisia wa vyanzo vilivyopo kabla ya kuweka kwenye mfumo.
Katika hatua nyingine ameelezea utaratibu wa kukusanya mapato kuwa ni kutambua chanzo husika, kumtambua mlipa kodi, kufanya tathmini ya kila chanzo, kutoa bili/Control namba, kulipa, kuwasilisha benki ndani ya saa 24 baada ya kukusanya, kutoa taarifa ya kimfumo, kufuatilia wadaiwa na kufanya mapitiao ya hatua zote kwa ajili ya maboresho huku akikisistiza kuwa malipo yote yanayolipwa yatolewe risiti ya kimfumo
Kwa upande mwingine amewakumbusha washiriki kuwa, katika suala la makusanyo ya ndani msamaha wa kutokulipa mapato au faini hutolewa na Waziri mwenye dhamana ya OR-TAMISEMI pekee na sio Madiwani na kwamba wao jukumu lao kubwa ni kuhamasisha kulipa na kuhuwisha sheria ndogo pale zitakapo kuwa zimepitwa na wakati kulingana na mahitaji
Washiriki wengine waliohudhuria mafunzo hayo ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde, Mkuu wa Idara ya utumishi na utawala Protas Dibogo, Gerald Mbosoli aliyefundisha somo la utekelezaji wa miradi kupitia mfumo wa force account na maandalizi na utekelezaji wa mpango wa bajeti pamoja Katibu tawala msaidizi anayeshughulikia masuala ya Serikali za Mitaa ndugu Yona Mwakilembe.
Haki Zote Zimahifadhiwa