Kibaha, Oktoba 16, 2025 — Msimamizi wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 Jimbo la Kibaha Mjini, Bi. Theresia Kyara, amewahamasisha watumishi wa umma pamoja na wananchi kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la upigaji kura litakalofanyika tarehe 29 Oktoba 2025, kwa ajili ya kumchagua diwani, mbunge na Rais.
Bi. Kyara ametoa wito huo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha katika ukumbi wa jengo la utawala, Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa hiyo, ambapo amesisitiza umuhimu wa watumishi wa umma kuwa mfano wa kuigwa kwa kushiriki kikamilifu katika zoezi hilo muhimu la kidemokrasia.
“Tunapowahamasisha wananchi kwenda kupiga kura, ni wajibu wetu sisi kama watumishi wa umma kuwa mstari wa mbele kuonesha mfano. Huu ni wakati wa kuamua hatma ya uongozi wa nchi yetu kwa kupiga kura kwa amani na utulivu,” alisema Bi. Kyara.
Aidha, alieleza kuwa maandalizi yote ya uchaguzi kwa ngazi ya jimbo yamekamilika, na kilichosalia ni wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi ili kutimiza haki yao ya kikatiba.
“Tunawasihi wananchi wote wa Kibaha Mjini mjitokeze kwa wingi tarehe 29 Oktoba. Maandalizi yamekamilika, tunachosubiri sasa ni siku yenyewe ya uchaguzi. Tujitokeze kwa wingi, kwa amani na utulivu, kuchagua viongozi tunaowataka kwa mujibu wa demokrasia yetu,” aliongeza.
Bi. Kyara pia amewahimiza watumishi wa Manispaa ya Kibaha kuendelea kutoa elimu kwa jamii inayowazunguka juu ya umuhimu wa kushiriki uchaguzi, ili kuhakikisha mwitikio mkubwa kutoka kwa wapiga kura wa Kibaha Mjini.
Haki Zote Zimahifadhiwa