NAIBU WAZIRI WA MIFUGO NA UVUVI ATOA MAAGIZO KWA TANESCO,DAWASA
Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Naibu Waziri wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega ametoa maagizo kwa taasisi za TANESCO na DAWASA za kuhakikisha wanafikisha huduma zao kwenye machinjio ya Mji Kibaha mara moja ili kurahisisha uendeshaji wa mtambo wa uchinjaji.
Ulega akiwa ameambatana na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Sara Msafiri, Mkurugenzi wa Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde na wataalam wa Wizara yake alipofanya ziara ya kikazi mwanzoni mwa wiki kukagua maendeleo ya sekta ya Uvuvi na Ufugaji kwenye Mkoa wa Pwani.
Evastus Mahuwi anayesimamia machinjio hayo amemweleza Naibu Waziri kuwa upatikanaji wa huduma ya Maji na nishati ya umeme hauridhishi hivyo kuathiri uchinjaji kwan mtambo huo unahitaji Maji mengi na nishati ya umeme kubwa ili kuendesha mtambo kuchinja na kuchakata kitoweo.
Mahuwi ameongeza kuwa ukosefu wa umeme umekuwa ni mzigo kwa Halmashauri kwani ili kupata kitoweo Safi hulazimika kununua Maji hali inayopelekea gharama za uendeshaji kuwa kubwa.
"Mhe.Naibu Waziri changamoto ya nishati ya umeme hapa ni kubwa,uliopo hapa hauendani na usanifu wa mtambo wetu hivyo mara nyingi tunatumia genereta hivyo tunaingia gharama nyingine ya kununua mafuta"
Mwenyekiti wa Rahma Foundation Abdulhimid Khan amesema kuwa uwepo wa Maji na nishati ya umeme ya uhakika machinjioni hapo inaweza kuwa fursa kwa makampuni mengine kuja kuwekeza viwanda vya kusindika nyama,soseji na kutengeneza vyakula vya Mifugo kwa kutumia malighafi za wanyama wanaochinjwa na kwamba hiyo itaongeza mnyororo wa thamani kwa wafugaji na kipato zaidi kwa Halmashauri.
Ulega ametoa maelekezo kwa niaba ya Serikali kwa TANESCO na DAWASA kufikisha huduma hizo ili kurahisisha uendeshaji kwani ni chanzo cha mapato ya Serikali yanayotukika kuhudumia wananchi
Mhandisi Godfrey Nathani aliyemwakilisha Meneja wa TANESCO amesema tayari bajeti ya kuunganisha kilovoti 33 kwenye transforma iliyopo machinjioni imeanza kutumika na suvei imeshafanyika hivyo wakati wowote tatizo litakoma.
Kwa upande wake Meneja wa matengenezo DAWASA Mhandisi Charles Kimario amesema mkakati walionao ni kujenga tenki kubwa la kuhifadhia Maji lenye ujazo la lita milioni 6 kwenye bajeti ya 2022/2023 litakalotumika kwenye kata ya Pangani ikiwemo machinjioni.
Mhandisi Mshamu Munde ambaye ndiye msimamizi wa shughuli za Maendeleo kwenye Halmashauri ya Mji Kibaha amemhakikishia Naibu Waziri kuwa ataendelea kufuatilia kwa karibu kwa taasisi hizo wezeshi ili huduma hizo zipatikane kwa wakati.
Haki Zote Zimahifadhiwa