Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuzindua kuanza kwa huduma ya usafirishaji wa mzigo kwa njia ya SGR katika bandari Kavu ya Kwala, Kibaha mkoani Pwani pia kuzindua kongani ya viwanda ambayo itakua na viwanda zaidi ya 200 mkoani humo.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukagua maandalizi ya uzinduzi huo katika eneo la Bandari Kavu ya Kwala, Kibaha Pwani , Julai 30, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge amesema uzinduzi huo utaambatana na upokeaji wa mabehewa ya treni ya SGR na upokeaji mabehewa ya mizigo ya treni ya MGR.
Mhe. Kunenge amesema uwekezaji huo mkubwa ni matokeo ya maono na miongozo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo yamewezesha kuweka mazingira wezeshi ya kisera kwa sekta ya viwanda na biashara akibainisha kuwa matarajio ya Serikali ni kupunguza msongamano wa makasha katika bandari ya Dar es Salaam kwa asilimia 30 pia msongamano wa malori kwenye barabara ya kuu inayoelekea mkoani Morogoro na ile ya TANZAM.
Ameongeza kuwa mradi huo utaongeza ajira kwa Watanzania, kukuza ukusanyaji wa mapato ya kodi na kuboresha ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini akibainisha kuwa eneo hilo lina nafasi ya kipekee kijiografia kutokana na kuunganishwa na miundombinu mbalimbali ya usafirishaji, jambo linalotarajiwa kuchochea biashara ya kimkakati kati ya Tanzania na nchi jirani.
“Bandari kavu ya Kwala imezungukwa na bandari kavu za nchi takribani 11 zinazotumia Bandari ya Dar es Salaam zikiwemo Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Malawi na nyingine za maziwa makuu ambazo tayari zina maeneo hapa, Kwala imeileta Jumuiya ya Afrika Mashariki na nchi za SADC hapa" amesema Mhe. Kunenge.
Mhe. Kunenge ametoa wito kwa wananchi wajitokeze kwa wingi katika hafla ya uzinduzi huo itakayofanyika Julai 31, 2025 akibainisha kuwa kongani ya viwanda na bandari kavu ya Kwala itakuwa na manufaa makubwa katika uchumi wa wananchi kupitia ajira na shughuli za ujenzi na usafirishaji.
Haki Zote Zimahifadhiwa