Na Byarugaba Innocent, Pwani
Wananchi wa Kata ya Mbwawa, halmashauri ya Mji Kibaha wamepaza sauti kwa Mkuu wa Mkoa huo Mhe.Abubakar Kunenge ya kujengewa wodi ya wazazi na kituo cha afya ili wapate staha na kustirika wakati wa kujifungua.
Kilio hicho kimetolewa kwenye mkutano wa kutatua kero za wananchi uliofanyika kwenye eneo la zahanati kongwe ya Mbwawa na kuhudhuria na mamia ya wananchi hivi karibuni.
Fatuma Matambo amesema hali ya wananchi kwenye huduma ya uzazi hairidhishi kwani wakati mwingine huifuata Kituo cha afya Mlandizi umbali wa KM 13 hali ambayo huchangia kusababisha vifo kwa wajawazito na watoto na kutumia fursa hiyo kuomba Uboreshaji wa huduma kwani idadi ya watu inazidi kuongezeka
Aidha,Asha Matago ambaye ni ana cheti cha ukunga wa jadi amesema kuwa wapo akina hutumia chumba kidogo kilichopo zahanati hapo lakini wanapofika wengi wenye kuhitaji huduma huwa kwenye Mazingira magumu ya kutafuta sehemu ya kuwaweka hali ambayo huwalazimu kuwapeleka vyumba vingine visivyokuwa na miundombinu ya uzazi.
Matago ameongeza kuwa wanapolazimika kuwapeleka kituo cha afya Mlandizi wengi kutokana na kuwa na uchungu tayari hujifungulia njiani ambapo kutokana na Mazingira kutokuwa rafiki hutokwa na damu nyingi,kupatwa na degedege na kupelekea vifo.
Deusi Zabloni ambaye ni Mwenyekiti wa Serikalini ya Mtaa wa Mbwawa amesema kuwa tangu Mwaka 2020 wamekuwa na nia ya kujenga wodi ya wazazi na tayari wameshakusanya tofali 6800 na wapo tayari kuchangia hata fedha ili kuokoa maisha ya wananchi wao lakini kikwako ni eneo dogo lililopo lenye Ukubwa wa ekari 6
Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Mhe.Sara Msafiri ameungana na kilio cha wananchi cha kujengewa wodi hiyo kwani wamekuwa wakitembea umbali mrefu kufuata huduma za kujifungua ingawa shida yao imekuwa na kutochangamka kupata eneo lenye Ukubwa unastahili ekari 15 na kuendelea kwa ajili ya Ujenzi wa Kituo cha Afya badala yake wanatamani eneo la ekari Sita litumike tofauti na miongozo ya Serikali.
Akiwatoa hofu wananchi,Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mhe.Kunenge amewaeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe.Samia Suluhu Hassan imeshatoa fedha kiasi cha Bilioni Mbili kwa ajili ya Ujenzi wa kituo cha afya Mbwawa lakini fedha hizo zinaweza kupelekwa kwingine kwenye uhitaji kutokana na eneo lao kuwa dogo hivyo amewapa siku nne kutafuta eneo linastahili kutokana na Vigezo vya Wizara ya afya.
"Mhe.Samia Suluhu Hassan falsafa yake ya Uongozi ni kuwatumikia wananchi, Wakati wote anafanyakazi ya kuondoa kero ili kuboresha maisha na kuleta Maendeleo ya wananchi nchini"
Aidha, Kunenge ameeleza kuwa miongoni mwa mambo anayoyapa kipaumbele Mhe.Samia ni kuwaondolea kero akina Mama hasa upande wa uzazi ili kupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito kwani hii ni changamoto kubwa kwenye ubinadamu.
Hata hivyo Kunenge ameruhusu Uongozi wa Serikali ya Mtaa kwa kushirikiana na wataalam wa Halmashauri kuanza ujenzi wa chumba cha kujifungulia kwa kutumia kiasi cha fedha shilingi milioni 9 zilizopo kwenye akaunti ya Serikali ya Mtaa na halmashauri itaendelea na ukamilishaji pale itakapofikia
Haki Zote Zimahifadhiwa