Bagamoyo, Tanzania – Timu ya ukusanyaji mapato ikiongozwa na Wakuu wa Divisheni na Vitengo kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo tarehe 21/07/2025 imefanya ziara ya kikazi ya siku moja katika Manispaa ya Kibaha kwa lengo la kujifunza mbinu bora za ukusanyaji wa mapato.
Ziara hiyo imelenga kubadilishana uzoefu na mawazo kuhusu namna bora ya kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri, kwa madhumuni ya kuboresha mifumo ya mapato na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Akizungumza wakati wa utambulisho, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo, Bw. Shauri Selenda, amesema kuwa ziara hiyo inalenga kujifunza na kupata uzoefu kuhusu mikakati na mbinu zinazotumika katika Manispaa ya Kibaha ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa katika ukusanyaji wa mapato.
“Tumeamua kuja kujifunza hapa Kibaha kwa sababu Manispaa hii imekuwa mfano wa kuigwa katika ukusanyaji wa mapato. Tunataka mbinu hizi nzuri zisaidie pia katika kuboresha ukusanyaji wetu Bagamoyo,” alisema Bw. Selenda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Kibaha Dkt Rogers shemwelekwa amesema Manispaa hiyo imejipambanua kama chuo cha utoaji wa elimu bora ya ukusanyaji wa mapato, na kupongeza Halmashauri ya Bagamoyo kwa hatua hiyo ya kujifunza kutoka kwa wengine.
“Manispaa ya Kibaha ni mahali pa kujifunza. Tuko tayari kuendelea kushirikiana na Halmashauri nyingine ili tuweze kuinua kiwango cha ukusanyaji wa mapato nchini,” alisema Mkurugenzi huyo.
Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuimarisha ukusanyaji wa mapato kwa Halmashauri zote nchini, kwa lengo la kufanikisha maendeleo endelevu na utoaji bora wa huduma kwa wananchi.
Haki Zote Zimahifadhiwa