UJENZI WA SOKO LA BILIONI 8 KIBAHA WAFIKIA ASILIMIA 95
Na. Innocent Byarugaba
Ujenzi wa Soko la Kisasa la halmashauri ya Mji Kibaha umefikia asilimia 95 ya utekelezaji wake ambapo kazi zinazoendelea ni umaliziaji. Soko hili linajengwa na Mkandarasi Elerai Construction CO. Ltd kwa Gharama za shilingi 7,298,549,844 pamoja na kodi ya ongezeko la thamani kwa kutumia fedha za Serikali Kuu.
Aidha, linasimamiwa na Mhandisi Mshauri M/S Luptan Consult and Mhandisi Consultancy ltd kwa gharama ya shilingi 294,410,000 kwa kutumia fedha za UNCDF hivyo kufanya gharama za Mradi kuwa jumla ya shilingi 7,592,959,844
Mradi huu wa soko ulianza kutekelezwa kuanzia tarehe 1/3/2019 na unategemea kukamilika muda wowote kuanzia sasa.
Mhandisi wa Halmashauri ya Mji Kibaha John Alexander amesema kuwa Soko hili kubwa la Kisasa litakuwa na huduma za Kibenki 2, ATM 12, Maduka 63 ya ukubwa mbalimbali kuanzia mita za Mraba 12 hadi 63, Ofisi za Utawala, Matundu 35 ya vyoo, Super Market 1, Mgahawa 1, Chumba cha huduma za akina mama na kizimba cha kukusanyia taka.
Mhandisi Alexander ameongeza kuwa eneo la chini (Basement) litakuwa na maduka/vizimba kwa ajili ya mabucha ya nyama na samaki pamoja na Soko la jumla la vyakula kama Ndizi, Viazi, Matunda na Nafaka
Aidha, kutakuwa na sehemu ya maegesho ya magari madogo 150 na makubwa15, Matanki ya kuhifadhia maji yenye ujazo wa Lita 110,000 na vyumba vitatu vya walinzi. Aidha kwa ajili ya kurahisisha kuingia na kutoka kutakuwa na mageti matatu.
Akielezea maendeleo ya mradi wa soko zima, afisa Mipango, takwimu na ufuatiliaji wa Halmashauri ya Mji Kibaha Wambura Yamo amesema kwa ujumla hali ya utekelezaji wa Mradi hadi sasa imefikia asilimia 95 ambapo kazi zinazoendelea ni umaliziaji wa jengo na kwamba mkandarasi atakabidhi muda wowote.
Wambura ameongeza kuwa Soko litatoa ajira kwa Wafanyabiashara 253, Aidha zaidi ya wananchi 2000 watapata huduma katika Soko hili huku Halmashauri inategemea kukusanya Mapato kiasi cha shilingi 281,424,000.00 kwa mwaka kutoka katika Soko hili hivyo kuongeza wigo wa Mapato ambayo yatatumika kuboresha huduma za Kijamii na kiuchumi kwa Wananchi wa Mji wa Kibaha ikiwa ni pamoja na kutoa Mikopo kwa makundi ya Watu wenye ulemavu, Wanawake na Vijana.
Mkurugenzi wa Halmashauri Mhandisi Mshamu Munde amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kujenga Soko hili la Kisasa na kuridhia Kiasi cha 8,000,000,000.00 kwa ajili ya ujenzi wake Aidha, hiki kitakuwa chanzo kizuri na endelevu cha mapato cha Mapato ya Halmashauri ya Mji Kibaha na kukuza uchumi wa Mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.
Haki Zote Zimahifadhiwa