HABARI: Vikundi vya Jogging Kibaha Vyafanya Mazoezi, Usafi na Uhamasishaji wa Uchaguzi Mkuu
Manispaa ya Kibaha, 18 Oktoba 2025 – Vikundi mbalimbali vya jogging katika Manispaa ya Kibaha leo vimefanya zoezi la mbio fupi pamoja na usafi katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kuhamasisha wananchi kufanya mazoezi ya mwili, kuchangia damu, kufanya usafi wa mazingira, na kushiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika tarehe 29.10.2025
Zoezi hilo lilianza saa 12 asubuhi katika eneo la Stand ya Maili Moja, kupitia Ofisi za NIDA, hadi Soko la Mnarani Loliondo, ambapo washiriki wamefanya usafi katika eneo la Mto Loliondo mara baada ya kumaliza mbio fupi.
Lengo kuu la zoezi hilo ni kuhamasisha wananchi kuzingatia afya kwa kufanya mazoezi ya mara kwa mara ili kuweka miili yao katika hali ya utimilifu, kushiriki shughuli za usafi wa mazingira kwa ajili ya kujikinga na magonjwa, pamoja na kuchangia damu katika vituo mbalimbali vya afya.
Vilevile, ni sehemu ya kuhamasisha jamii kushiriki kikamilifu zoezi la uchaguzi mkuu utakaofanyika tarehe 29 Oktoba 2025 kwa kuhamasisha wananchi wajitokeze kwa wingi kupiga kura.
Akizungumza katika tukio hilo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Kibaha Dkt Catherine Saguti amewapongeza washiriki wote kwa kujitoa kwao na uzalendo waliouonesha
.Amewataka wananchi waendelee kuwa mabalozi wa usafi wa mazingira na afya, pamoja na kushiriki kikamilifu uchaguzi Mkuu kwa kuwahamasisha wengine kujitokeza kupiga kura.
Aidha ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya Afya uliofanyika na Wananchi wa Manispaa ya Kibaha wananufaika na uwekezaji huu Kwa kupata huduma Bora za Afya.
“Tunawashukuru kwa moyo wenu wa uzalendo. Mazoezi ni tiba, usafi ni kinga, na uchaguzi ni haki. Tuwe sehemu ya mabadiliko kwa vitendo,” alisema Mganga Mkuu huyo.
Kwa upande wao, baadhi ya wananchi waliojitokeza kwenye zoezi hilo wamesema kuwa wameamua kuonesha mfano kwa jamii kwa kuchukua hatua badala ya maneno tu. Wamesisitiza umuhimu wa kujitolea katika shughuli za kijamii kama njia ya kuleta maendeleo ya pamoja.
Zoezi hili limepata muitikio mkubwa kutoka kwa wakazi wa Kibaha, na linatarajiwa kuendelea katika maeneo mengine ya manispaa hiyo katika wiki zijazo.
Haki Zote Zimahifadhiwa