Na Byarugaba Innocent,Mwanza
Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha wamekuja na mkakati mpya wa kuwasaidia wafanyabiashara ndogondogo na wale wanaotembeza 'Machinga' ili waweze kuendesha biashara zao kwa mafanikio zaidi na kuleta tija kwenye familia zao na Taifa kwa Ujumla
Mawazo ya kuwaboreshea zaidi wafanyabiashara zao yameibuliwa wakati wa ziara ya kubadilishana Uzoefu iliyofanyika Novemba 3,2022 Jijini Mwanza
Meya wa Jiji la Mwanza Mhe.Sima Constantine amesema katika kukabiliana na wimbi kubwa la wafanyabiashara wadogo wakiwemo wanaotembeza bidhaa mitaani,wameanza ujenzi wa Soko kubwa litakalogharimu kiasi cha Bilioni 23 fedha kutoka Serikali kuu na linatarajia kukamilika Machi,2023 likiwa na uwezo wa kuwahudumia wafanyabiashara zaidi ya 2000.
Aidha,Afisa Mipango wa Jiji la Mwanza Akim Albert amebainisha kuwa Soko likiwa na Maduka 400,Vizimba 500,nafasi za wamachinga 500,stoo 10,Mama na Baba lishe 20 na wauza mbogamboga 700.
Denis Muhoja,Afisa Maendeleo ya jamii Jiji la Mwanza akitoa Uzoefu wa namna walivyowapata wafanyabiashara wadogo takribani 12,000 na kuwaweka kwenye Maeneo maalum amesema kazi ya kwanza ni kuwatambua,kuwaweka kwenye kanzidata na kufanyanao vikao mara kwa mara ili kufikia muafaka na baada ya hapo ni kufanya utekelezaji wake.
Akitoa neno la shukrani kwa Uzoefu walioupata, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhe.Mussa Ndomba ameeleza kuwa Halmashauri ya Mji Kibaha tayari imetenga eneo maalum la wafanyabiashara hao Mtaa wa Zegereni litakalopangwa kisekata kutokana na Biashara zao na anaamini kuwa endapo watakubali kwenda wanaweza kukuza mitaji yao na kuwafanya wafanyabiashara wakubwa na walipa kodi wazuri hivyo kuleta tija kwa Taifa.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha Mhandisi Mshamu Munde ameeleza maandalizi ya awali ya kuandaa eneo hilo maalum yameanza na ametoa rai kwa Kaimu Mkuu wa Idara ya Viwanda,Biashara na Uwekezaji Adolf Msangi kuanza kuwatambua na kuandaa kanzidata kutokana na bidhaa zao itakayotumiwa wakati wa kuwapanga.
Haki Zote Zimahifadhiwa