Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt. Rogers Shemwelekwa Atembelea Wafanyabiashara Ndogo Pembeni mwa Barabara
Kibaha, 16 Septemba 2025 — Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, ametembelea wafanyabiashara wadogo wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara katika kata mbalimbali za Manispaa hiyo na kufanya nao kikao kazi chenye lengo la kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo na kuangalia namna bora ya kuzitatua.
Kikao hicho kilichofanyika kwa nyakati tofauti katika kata za Maili Moja, Tumbi, Sofu na Picha ya Ndege, kililenga kuimarisha mahusiano kati ya uongozi wa Manispaa na wafanyabiashara wadogo pamoja na kuweka mikakati ya kuwawezesha kiuchumi.
Akizungumza na wafanyabiashara hao, Dkt. Shemwelekwa amewataka kuunda vikundi vya watu watano watano ili waweze kunufaika na mikopo isiyo na riba inayotolewa na Manispaa ya Kibaha kwa makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Aidha, amewataka kutolipa ushuru kutokana na mazingira wanayofanyia biashara kutopangwa rasmi, huku akiwahakikishia kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya ujenzi wa masoko ya kisasa yatakayowapokea na kuwawezesha kufanya biashara katika maeneo rasmi, salama na yenye miundombinu bora.
“Ni muhimu mkajipanga mapema kwa kuunda vikundi ili mkikopesheka na mnufaike na mikopo inayotolewa na Manispaa. Serikali ipo pamoja nanyi na ndio maana tumeamua kuwafuata mlipo ili tushirikiane kuboresha maisha yenu,” alisema Dkt. Shemwelekwa.
Kwa upande wao, wajasiriamali hao wamempongeza Mkurugenzi huyo kwa kuwafikia moja kwa moja na kuonesha nia ya dhati ya kushughulikia changamoto zao, huku wakieleza kuwa huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano kati yao na uongozi wa Manispaa.
“Tunaona fahari sana kutembelewa na Mkurugenzi wetu. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu kuja kusikiliza changamoto zetu moja kwa moja. Tunampongeza sana,” alisema mmoja wa wafanyabiashara katika Kata ya Tumbi.
Ziara hiyo imeonyesha dhamira ya Manispaa ya Kibaha katika kuimarisha ustawi wa wafanyabiashara wadogo na kuweka mazingira bora ya biashara kwa kila mwananchi.
Haki Zote Zimahifadhiwa