WALIOVAMIA ENEO LA MWEKEZAJI WAMWOMBA MKURUGENZI AWASAIDIE WASIVUNJIWE
Na Byarugaba Innocent,Kibaha
Wakazi wa mitaa ya Viziwaziwa,Mikongeni na Sagare halmashauri ya Mji Kibaha Mkoani Pwani ,wamemwomba Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuwafikishia ombi la kupunguziwa bei ya Ardhi kutoka shilingi 15,000 kwa mita mraba anazotaka kulipwa mwekezaji kwenye eneo walilovamia hadi shilingi 2500/- kiwango wanachodai kuwa wanauwezo nacho kulipia.
Ombi hilo limetolewa Agosti 26,2022 wakati wa Mkutano baina yao na Uongozi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha uliofanyika Viziwaziwa ikiwa ni mwendelezo wa mikutano kadhaa ambayo imekuwa ikifanyika ili kutafuta suluhu ya Mgogoro wa ardhi hiyo kwa zaidi ya Miaka 10 Sasa ambapo wananchi hao wanadaiwa kuvamia na kuweka Makazi
"sisi tuliingia hapa kama mafuriko wengi tulitapeliwa kwa kuuziwa eneo hilo bila kujua.Tumeshakaa kwa miaka mingi hivyo tunakuomba Mkurugenzi tufikishie ombi letu kwa mwekezaji la kupunguziwa bei,"amesema Innocent Kimaro.
Aidha,Geoffrey Mfugale amesema kuwa ni vema mwekezaji huyo akawapunguzia kiwango cha bei kufikia 2500 kwani wakazi wengi wa mitaa hiyo vipato vyao ni duni na kwamba hawawezi kumudu gharama zinazotakiwa na mwekezaji.
Kwa upande wake Franza Teve amesema kuwa Mgogoro huo umekuwa ukiwasumbua kwa miaka mingi na wametumia gharama kubwa kutafuta suluhu na mwisho mwekezaji ameonekana ana haki hata hivyo bado wananchi wanaomba wapunguziwe,walipe ili waweze kupata uhalali wa umiliki wa maeneo hayo ili waishi kwa amani.
Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi amewaeleza wavamizi hao kuwa bei elekezi ya Ardhi kwa eneo la Viziwaziwa ni kati ya shilingi 5000-6000 ambapo Ardhi kwa matumizi ya Makazi pekee ni 5000 huku Makazi na Biashara ikiwa ni 6000.
Mkurugenzi wa halmashauri ya Mji wa Kibaha Mhandisi Mshamu Munde ameahidi kufikisha ombi lao kwa mwekezaji huku akitoa rai kwa wananchi hao kuangalia viwango na uhalisia wa thamani ya ardhi wanapopeleka ombi lao kama kweli wanataka kupunguziwa.
Eneo hilo lenye Ukubwa wa ekari 118 liliingia kwenye Mgogoro Mwaka 2014 baada ya wananchi kuvamia Ardhi na kuweka Makazi ya kudumu jambo ambalo ililazimika kufikishwa mahakamani na hatimaye mwekezaji akashinda kesi na wananchi kushindwa hali ambayo imetoa Kiashiria cha kutafuta njia ya maridhiano nje ya mahakama.
Zaidi ya kaya 581 zimejiandisha kukusudia kulipia gharama za maeneo au Viwanja wanavyohodhi iwapo mwekezaji atawalegezea bei na kufikia shilingi 2500.
Haki Zote Zimahifadhiwa