Wazee 160 Uyaoni Waadhimisha Siku ya Wazee kwa Kupima Afya Kibaha
Kibaha, 01 Oktoba 2025 — Wazee 160 kutoka Mtaa wa Uyaoni, Kata ya Mailimoja, Manispaa ya Kibaha wameadhimisha Siku ya Wazee Duniani kwa kupima afya zao na kupata elimu juu ya lishe na magonjwa yasiyoambukiza.
Maadhimisho hayo yalifanyika tarehe 01 Oktoba 2025, yakilenga kuboresha afya na ustawi wa kundi hilo muhimu katika jamii.
Wataalamu wa afya kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wametoa huduma mbalimbali ikiwemo upimaji wa hali ya lishe, kisukari, na shinikizo la damu. Aidha, wazee walipatiwa elimu ya lishe bora na namna ya kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza, hatua iliyolenga kuwawezesha kuishi maisha marefu yenye afya.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo ni Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, ambaye aliwakilishwa na Afisa Tarafa ya Kibaha, Bi Catherine Njau. Akizungumza katika hafla hiyo, Bi Njau amewapongeza wazee kwa kujitokeza kwa wingi na kuadhimisha siku yao kwa njia ya kuhamasisha afya, mshikamano, na ushiriki katika shughuli za kijamii.
“Mmeonesha mfano wa kuigwa. Tunaomba mzidi kushirikiana na viongozi katika kuleta maendeleo kwa kutoa ushauri wa busara kutokana na uzoefu wenu mkubwa,” alisema.
Aidha, amehimiza viongozi wa kata na mitaa kuhakikisha wazee wanashirikishwa kikamilifu katika kamati mbalimbali, hasa kwa kuwa baadhi yao walikuwa watumishi katika sekta muhimu kama afya, ulinzi na maendeleo ya jamii, na wana uwezo wa kuchangia uboreshaji wa huduma na usalama.
Kwa upande wao, wazee wa Mtaa wa Uyaoni wameiomba serikali kuwawezesha kufikiwa na mikopo kutoka taasisi za kifedha, na mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri iwaguse wazee.
Pia wameiomba serikali iwajengee zahanati katika mtaa huo au kuwawekea kituo cha huduma ya kwanza, wakibainisha kuwa miongoni mwao wapo madaktari wastaafu ambao wanaweza kutoa huduma kwa urahisi kwa wenzao.
Mtendaji wa Mtaa wa Uyaoni, Bi Aminata Nombo, alithibitisha kuwa jumuiya hiyo ya wazee ina umoja wa watu 160 ambao wanashirikiana kwa karibu na kushikamana katika masuala ya kijamii.
Maadhimisho haya yameonesha umuhimu wa kuwatambua na kuwawezesha wazee kama sehemu muhimu ya maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Haki Zote Zimahifadhiwa