Aliyosema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan
#Huko miaka ya nyuma UCSAF mlikuwa mnajenga minara 30 wakati mwingine 50 lakini sasa mnatarajia kujenga minara zaidi ya 700 sio kazi ndogo, lazima Rais niwepo katika kushuhudia mikataba ikisainiwa.
#Nawashukuru watoa huduma katika mradi huu hasa Shirika la TTCL na Makampuni ya simu kwa ushirikiano mkubwa wanaotoa kwa Serikali yetu. Pia, natoa shukrani maalumu kwa Benki ya Dunia ambayo imeendelea kutuunga mkono katika mradi huu na mingine ya maendeleo katika nchi yetu.
#Nimetoa pongezi nyingi kwa utekelezaji wa mradi huu kwa vile sasa mikoa yote 26 ya Tanzania bara inakwenda kupata huduma bora za mawasiliano baada ya Zanzibar kufikiwa na huduma hii mwezi Novemba, 2022.
#Huu ni utekelezaji mzuri wa ahadi niliyokuwa nikitoa mara kadhaa napokutana na wananchi niliahidi kukuza na kuimarisha Sekta ya TEHAMA ili kutoa ajira kwa vijana na kusukuma maendeleo ambapo mradi huu ni utekelezaji mmoja wapo wa ahadi hiyo.
#Kuwepo kwa huduma bora za mawasiliano, hususani katika maeneo ya vijijini, ni muhimu sana kiuchumi, kisiasa, kijamii, kiutamaduni na hata katika masuala ya ulinzi na usalama kwa nchi yetu, tulichokishuhudia leo ni kichocheo kikubwa cha mafanikio kwani huwezesha sekta zote kukua.
#Tutamaliza kadhia ya mawasiliano vijijini, tunakwenda kukuza biashara na kutafuta soko kwa uhakika. Kila mmoja awe Mkulima, Mwalimu na wananchi wote waliopo Vijijini watakuwa na taarifa kwenye viganja vyao
#Jambo kubwa zaidi, tunaenda kubadilisha teknolojia vijijini, kwa sasa hivi wakulima wetu wana simu maarufu kwa jina la ‘vitochi’ lakini tutakapoimarisha mitandao yetu na upatikanaji wa huduma za mawasiliano, wakulima watatoka kwenye tochi kwenda kwenye tachi.
#Simu za tachi ndizo zitakazowapa taarifa zote za nchi na za Dunia, kwa hiyo tunakwenda kupeleka ukuaji wa teknolojia kule vijijini.
#Moja ya huduma za mawasiliano zinayofanywa na UCSAF, ni kuimarisha huduma za matibabu mtandao ‘Telemedicine’ kwenda vijijini, huduma hizi zitatusaidia kupunguza vifo vya mama na watoto wakati wa kujifungua
#Mradi mkubwa wa M-Mama ambao tuliuanza Tanzania na sasa unaigwa na nchi nyingine za Afrika, kwa kutumia mitandao hii tunakwenda kupunguza vifo vya mama na watoto na mambo makubwa zaidi yatatokea ndani ya Sekta ya Afya kwa kutumia mitandao hii.
#Mitandao na mifumo ikikaa vizuri, tutaweza kusimamia vyema matumizi ya dawa na vifaa tiba, hivyo kukuza pia huduma kwa wananchi.
#Nawaomba wananchi watoe maoni yao kwa jinsi wanavyoona mitaala yetu ya elimu itaendelea vizuri, hii TEHAMA itakwenda kukuza elimu kwa watoto wetu, Itaimarisha usalama kwa sababu ya kuwepo kwa mawasiliano, hivyo lolote litakalotokea kuanzia ndani ya vijiji kwenda kata, wilaya, mkoa au taifa moja kwa moja na hatua zikaweza kuchukuliwa kwa haraka.
#Kwa kufanya hivyo, tunatekeleza malengo ya Milenia tuliyowekewa, lengo Namba 2 la Afya, Namba 4 la Elimu na lengo Namba 10 la kuleta usawa kwa mijini na vijijini kwa mambo mbalimbali ikiwemo kupata taarifa kwa Watanzania.
#Kuna lengo Namba 16 ambalo linaeleza jinsi ya kutumia huduma na kuongeza uzalishaji, natoa rai kwa wananchi wa vijijini kutumia mitandao zaidi kuondoa changamoto walizonazo huko na kuongeza uzalishaji.
#Tutaongeza matumizi ya mitandao kwa huduma za fedha, Tanzania ina sifa ya kuwa na idadi kubwa ya watu wanaotumia simu kutuma fedha kwa sababu ya kupanuka kwa huduma za mitandao.
#Tunachokifanya leo, kinagusa sekta mbalimbali za nchi yetu, tutakuza maendeleo mijini na vijijini ili wote twende kwa kasi, si jambo dogo ni kubwa sana ndio maana nimesema niwepo ili nishuhudie.
#Fedha tunazozitoa ni ruzuku kutoka Serikalini, lakini kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 26.36 ambazo ni sawa na fedha za kitanzania Shilingi bilioni 60.7, ni mkopo kutoka Benki ya Dunia na Shilingi bilioni 70.16 zinatokana na tozo zinazolipwa na makampuni ya simu kwa Mfuko wa UCSAF
#Miradi hii ya ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi, inatoa msukumo mzuri wa maendeleo, hivyo nawaomba sekta nyingine ziige mfano huo. Utekelezaji wa mradi huu ni hatua muhimu sana katika kuelekea Mapinduzi ya Nne ya Maendeleo ya Viwanda ambayo msingi wake ni kufikia uchumi wa kidijiti unaoifanya Sekta ya Mawasiliano kuwa nyenzo wezeshi kwa maendeleo ya sekta zote ndani ya nchi yetu.
#Kukamilika kwa mradi huu, kutasaidia sana kukuza Pato la Taifa kutokana na kuongezeka kwa wigo wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) pamoja na Mawasiliano katika sekta nyingine.
#Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, ripoti inasema usikivu wa simu katika maeneo ya vijijini umeongezeka na kufikia asilimia 97 ikilinganishwa na asilimia 45 ya mwaka 2009.
#Natoa maelekezo, na tutaitana na wahusika wote wa kutoa vibali, nataka vibali hivi vya mradi uliosainiwa leo visizidi mwezi mmoja kutoka leo tarehe 13/05/2023, nitamuuliza Waziri husika inapofika tarehe kama ya leo mwezi ujao.
#Suala lingine ni maeneo yetu ya kijiographia na kipato kidogo cha wakazi wa baadhi ya maeneo. Najua kuna maeneo yapo ndani sana ambapo mjengaji wa minara hafiki nawaomba wana mtandao wa mashirika ya simu, kuja na teknolojia ya gharama nafuu ambayo inaweza kuwafikia kundi hilo ili na wao waweze kutumia huduma za mtandao.
#Nawatia moyo kundelea kupeleka huduma bila malipo kwa baadhi ya makundi kwa mfano madaktari wanaotumia huduma ya Telemidicine, pia maeneo ya Vyuo kama UDOM nao wanapatiwa huduma ili wanafunzi waweze kufanya vizuri kwenye masomo yao, nawaomba muendelee na kwenye maeneo mengine muhimu na muangalie namna ya kufidia gharama hizo.
#Natoa wito kuendelea na mchakato wa kupeleka huduma za mawasiliano vijijini ili zile Kata zilizobakia ambazo minara yao haikusainiwa leo hapa na zenyewe zipate huduma hii kwa haraka.
#Tunapaswa kuilinda minara hii, inajengwa kwa gharama kubwa, hivyo kwenda kufanya uharibifu wowote ni kwenda kuhujumu maendeleo tunayoyapeleka vijijini. Nawaomba sana wale wanaosimamia kuhakikisha minara hii na miradi mingine yote ya Serikali inabaki kuwa salama.
#Natoa maagizo kwa Makampuni ya Simu, kuhakikisha kuwa minara yote inakamilika kwa mujibu wa mikataba, kwa ubora, vigezo na wakati. Kwa upande wa Serikali tunakwenda kupunguza urasimu ili vibali vitoke mapema. Halmashauri na Taasisi zote zinazohusika na utoaji wa vibali ndani ya mwezi mmoja vibali vyote viwe vimetoka.
#Naagiza Mfuko wa UCSAF ushirikiane na TARURA kuhakikisha njia zinapatikana katika maeneo ya vijijini inapokwenda kujengwa minara hiyo. Vile vile, REA pamoja na changamoto ya fedha mliyonayo ya kupeleka umeme kwenye vitongoji hakikisheni mnafikisha umeme sehemu zote ambazo minara hii itajengwa, hii itatusaidia kushusha gharama za mabando tunazotumia.
#Naelekeza UCSAF kuendelea kushirikiana na taasisi nyingine za Serikali kupanga mipango ya pamoja ili kuondoa changamoto zinazoweza kujitokeza.
#Waziri Nape Nnauye, nakuagiza kuangalia vyema Mfuko huu ili nao wakatimize majukumu yao tuliyowaelekeza wakafanye.
#Mashirika ya Simu najua mnatengeneza faida nzuri sana, angalieni namna ya kurudisha kwa jamii ili nao wafaidike na tujue shirika gani limefanya nini kwa wananchi, mnaweza hata kutuchangia katika mradi wa mitandao mashuleni tukaongeza nguvu ili twende pamoja.
#Wito wangu kwa vijana ni kutumia mitandao hii vyema kwa maendeleo yao, kulinda mila na silka zao, kutumia kujielimisha zaidi kuliko matumizi mengine yasiyo na manufaa.
Aliyosema Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson
#Nakupongeza Rais, Mhe. Dkt. Samia kwa kuchukua hatua ya kuirejesha Tume ya Mipango ambayo italisaidia Taifa kusonga mbele kwa kuunganisha sekta mbalimbali.
#Tunaamini kwamba, gharama katika matumizi ya mitandao itapungua kupitia minara hii inayopelekwa katika maeneo ya vijijini, minara hii ikiunganishwa na sekta ya nishati ikapeleka umeme vijijini, fedha za uendeshaji wa minara itakuwa ndogo, hivyo kushusha gharama za matumizi ya simu.
Aliyosema Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa
#Mradi wa ujenzi wa minara 758 nchini, utajibu ushauri na maswali ya Wabunge kuhusu nini mpango wa Serikali wa kumuwezesha Mtanzania kushika chombo cha mawasiliano na kuzungumza kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza, sasa mawasiliano yatasambaa nchi nzima.
#Natoa wito kwa Makampuni ya Mawasiliano Tanzania kuendelea kuweka mitaji zaidi kwa kuwa Serikali itaendelea kuwapa ushirikiano wakati wote kuhakikisha kwamba suala la mawasiliano linaimarika.
Aliyosema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye
#Kwa upande wa Zanzibar, kazi ya ujenzi wa minara ilifanyika mnamo Novemba, 2022 ambapo jumla ya minara 42 ilijengwa katika Shehia 38 Unguja na Pemba ambapo Serikali ilitoa ruzuku ya Shilingi bilioni 6.9 na kupelekea upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa jamii Zanzibar kufikia asilimia 99 kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi 2022.
#Kupitia UCSAF, Serikali imefanikiwa kufikisha huduma za mawasiliano kwa Watanzania takriban milioni 15 wanaoishi vijijini kupitia miradi mbalimbali inayotejelezwa na UCSAF kwa pamoja na Makampuni ya Simu.
#Serikali kupitia UCSAF imeingia makubaliano na watoa huduma kufikisha huduma za mawasiliano vijijini katika kata 1,258 zenye jumla ya vijiji 3,704 na wakazi 15,194,118 ambapo jumla ya minara ya mawasiliano 1,380 itajengwa.
#Katika mikataba 19 ambayo Mfuko wa UCSAF umeingia na Watoa Huduma za Mawasiliano, Serikali imeweza kutoa ruzuku ya Shilingi bilioni 199.9, fedha hizi ni ushahidi wa Serikali inavyothamini na kuhakikisha kila Mtanzania hasa wa vijijini wanapata mawasilano.
#Katika miradi ya aina hii, Serikali imekuwa ikitoa ruzuku ya wastani wa asilimia 40 na Watoa Huduma huchangia asilimia 60 ya gharama nzima ya mradi iliyobaki ambapo kwa wastani, gharama za kujenga mnara mmoja ni milioni 300 hadi 350.
#Tunapoelekea kwenye uchumi wa kidijitali, tunatamani twende wote kama nchi bila kumuacha mtu yoyote ndio maana Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kufikisha huduma za mawasiliano vijijini.
#Minara 758 itajengwa katika mikoa 26 ya Tanzania bara, vijiji 1,407 katika Kata 713 zilizopo katika Wilaya 127 ambapo hadi kukamilika kwake, Watanzania waishio vijijini wapatao 8,512,952 watafikiwa na huduma ya mawasiliano.
#Baada ya kukamilika kwa mradi huu utakaotekelezwa kwa takriban miezi 18, tunatarajia huduma za mawasiliano katika maeneo yanayokusudiwa, utachochea maendeleo katika maeneo hayo.
#Ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2022 iliyochambua jumla ya nchi 198 na ikaziweka nchi 69 ikiwemo Tanzania kuwa miongoni mwa vinara duniani katika mabadiliko ya kidijitali katika sekta ya umma.
#Katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wako Rais Samia, umeongoza mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita kurejea katika ushiriki wa shughuli za kisekta za mawasiliano za kimataifa ambapo imewezesha Tanzania kuchaguliwa kuwa katika taasisi kadhaa za kimataifa.
#Kuheshimika huku kwa Tanzania kimataifa, kumetokana na Tanzania kutambulika kama moja ya nchi zinazoendele barani Afrika katika suala la kutumia mifumo ya kidijitali kutoa huduma kwa jamii na jitihada za Tanzania katika kushiriki shughuli zote hizo.
Aliyosema Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mohammed Khamis Abdulla
#Leo Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan utashuhudia utiaji saini wa mikataba ya ujenzi wa minara 758 pamoja na kuongeza nguvu minara 304 ambapo utekelezaji huo ni matokeo ya ushirikiano baina ya Serikali, wadau wa maendeleo na Watoa Huduma za Mawasiliano katika kutekeleza Sera ya TEHAMA ya Mwaka 2016 pamoja na mikakati yake.
Aliyosema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule
#Minara hii inayoenda kujengwa katika maeneo ya vijijini ni mafanikio makubwa kwa kuwa yanaifungua nchi kwa kiwango cha hali ya juu, tunakupongeza Rais, Mhe. Samia kwa kazi unazozifanya ikiwemo hii ya mawasiliano.
#Mkoa wa Dodoma tulikuwa tunataka tupate programu ambayo itatumika kusimamia miradi tukiwa ofisini ili siku tukienda kufanya ziara katika miradi hiyo tukute kuna hatua imefikiwa sasa programu hii isingewezekana bila kupeleka mawasiliano katika maeneo ya vijijini ambapo miradi inatekelezwa.
#Ujenzi wa minara hii utasaidia kila sekta iimarike kupitia matumizi ya TEHAMA. Aidha, vishikwambi vilivyogawiwa kwa Walimu kuna maeneo vilikuwa havitumiki kwa sababu ya ukosefu wa mawasiliano, hivyo kupatikana kwa mawasiliano vishkwambi hivyo vitatumika kama ilivyokusudiwa.
Aliyosema Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Justina Mashiba
#Tulitangaza zabuni ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo 763 na baada ya mchakato huo, tulipata maeneo katika Kata 713 ambayo minara ya mawasiliano 758 itajengwa, hii ni historia.
#Ushiriki wa Watoa Huduma katika zabuni hii wameweza kushiriki kwa asilimia 93, hii pia ni historia iliyowekwa katika ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi.
#Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) litajenga minara katika Kata 104, Kampuni ya Vodacom Tanzania itajenga minara 190 katika maeneo mbalimbali, Kampuni ya Airtel Tanzania itajenga minara katika Kata 168, Kampuni ya Tigo Tanzania itajenga minara 262, Kampuni ya Viettel Tanzania itajenga minara 34 katika maeneo mbalimbali.
#Mbali na kujenga minara mipya, tutaongeza nguvu katika minara 304 ambayo ilikuwa ikitoa teknolojia ya 2G ambapo Kampuni ya Tigo Tanzania itaongeza nguvu katika minara 148, TTCL itaongeza nguvu katika minara 55, Kampuni ya Airtel minara 32 na Kampuni ya Vodacom minara 69.
#Tangu Taasisi ianze mwaka 2009, UCSAF imefanikiwa kujenga minara mingi ambayo ipo katika hatua mbalimbali, tumepeleka vifaa mbalimbali vya TEHAMA katika shule mbalimbali ikiwemo Kompyuta 4,750. Aidha, tumeanzisha huduma ya Tiba Mtandao ambayo lengo lake ni kuwasaidia Watanzania kupata huduma mbambali kutoka kwa wataalam wa afya bila kufika hospitali.
#Tunaendelea kujenga vituo vya TEHAMA katika maeneo mbalimbali, Zanzibar tumejenga vituo hivyo katika wilaya zote 11, kwa upande wa Tanzania Bara, tunashirikiana na Shirika la Posta katika kuhakikisha maeneo yao ya posta tunayawekea vituo vya TEHAMA ili kusaidia Watanzania wanapata huduma hizo.
#Nchi yetu imepakana na nchi nane hivyo ina mipaka nane, ni jukumu letu UCSAF kuangalia namna ya kupeleka huduma za mawasiliano katika maeneo ya mipaka, maeneo ya mbuga za wanyama pia yatapelekewa mawasiliano, vilevile, kuweka mawasiliano katika barabara kwa ajili ya usalama.
#Tunataraji kuanzisha Redio Jamii kwenye halmashauri zote nchini pia, tutaweka "wi-fi" katika maeneo ya wazi na maeneo ya vyuo vikuu nia ikiwa ni kuendelea kurahisisha mawasiliano.
Aliyosema Mkurugenzi wa Benki ya Dunia Nchini Tanzania, Nathan Belete
#Tunafahamu kwamba maendeleo ya TEHAMA yameleta mafanikio makubwa ya mawasiliano ndani ya nchi na dunia nzima, kupitia TEHAMA hata ufanisi katika biashara umeimarika na pia TEHAMA imeongeza fursa za kibiashara.
#Katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania, upatikanaji wa mawasiliano sio mkubwa, hivyo kupitia ujenzi wa minara hii, zaidi ya wananchi milioni 3 wataweza kupata intaneti ya kasi na kuweza kutumia vifaa vya kidijitali.
#Benki ya Dunia imeendelea kuisaidia nchi ya Tanzania katika sekta mbalimbali, kwa upande wa sekta ya mawasiliano, ufadhili wa Benki hiyo katika Mradi wa Kidijitali Tanzania ni Dola za Kimarekani milioni 50.
#Mradi huu ambao mkataba wake unasainiwa leo, Benki ya Dunia imefadhili takribani asilimia 20 ya fedha zitakazotumika katika mradi huo kwa ajili ya miundombinu ya kidijitali na maunganisho ya mitandao.
#Mradi huu utasaidia zaidi ya minara 1000 kujengwa na kuongezwa nguvu katika maeneo ya vijijini, tutasaidiana na sekta binafsi kuongeza ufanisi wa mtandao kwa watanzania takriban milioni 3 kuifikia kasi ya 4G, mradi pia utaunganisha Wizara zote na taasisi zote za Serikali katika mtandao wa kasi ya juu.
Aliyosema Mwakilishi wa Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano Tanzania (TAMNOA), Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Vodacom Tanzania, Philip Besiimire
#Tunaishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutambua kuwa uchumi wa kidijitali ni nyenzo muhimu kwa ukuaji na ustawi wa Tanzania ijayo na sisi kama Chama cha Watoa Huduma za Mawasiliano Tanzania, tumejidhatiti kushirikiana katika utekelezaji.
#Kwa umoja wetu tumekuwa mstari wa mbele kutoa huduma jumuishi za mawasiliano na kifedha nchini huku tukiwaunganisha na kuwawezesha Watanzania kwa nyenzo muhimu ili kumudu uchumi wa kidijitali.
#TAMNOA imewekeza jumla ya Shilingi trilioni 6.5 nchini na kuwezesha mawasiliano kwa wateja zaidi ya milioni 60 na tunaendelea kuboresha miundombinu ya mitandao yetu kwa kupanua upatikanaji wa intaneti ya uhakika na yenye kasi.
#Kupitia ushirikiano wetu na UCSAF, tumejenga minara ya mawasiliano zaidi ya 1,380 ambayo imeongeza upatikanaji wa huduma kwa jamii zilizo pembezoni kwa kuunganishwa na huduma mbalimbali za mawasiliano.
#Aidha, tumewekeza Shilingi bilioni 350 kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaowezesha Watanzania wengi kuunganishwa kwa haraka na huduma za mawasiliano.
Aliyosema Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo
#Naipongeza Serikali kwa kuchukua uamuzi huu muhimu ambao unatekeleza Ilani ya Chama Tawala mwaka 2020/25 kwa kiwango kikubwa kinachofikia zaidi ya asilimia 90.
#Teknolojia inarahisisha shughuli nyingi, Chama Tawala kitatoa Kompyuta 50 ili kuweka chachu ya msukumo wa utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala kwenye eneo la teknolojia ya habari na mawasiliano kwenye shule zetu nchini.
IMEANDALIWA NA IDARA YA HABARI - MAELEZO
Haki Zote Zimahifadhiwa